WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote wahakikishe wanaboresha mshikamano wao pamoja na kuimarisha uzalendo kwa Taifa lao.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Agosti 20, 2017) wakati akizungumza na
wanafunzi wa Kitanzania wanaosomea udaktari nchini Cuba.
Waziri
Mkuu yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi
yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Alisema uzalendo
kwa Taifa ni jambo muhimu.
“Uzalendo ni muhimu sana
kwa sababu tumekosa fursa nyingi za kimaendeleo kutokana na baadhi ya wananchi
kutokuwa wazalendo kwa Taifa lao.”
Kutokana na hali hiyo Serikali inawasisitiza Wananchi kuwa wazalendo
na washirikiane kuhakikisha fursa za kimaendeleo zilizoko nchini zinaendelezwa.
Alisema Serikali inatekeleza miradi mingi kwa lengo la kukuza
uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati, ni vema wananchi wakashirikiana nayo ili
kufanikisha adhma hiyo.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi hao
kuzingatia sheria za nchini waliyoko pamoja na kukumbuka kurudi nyumbani mara
wamalizapo masomo yao.
Alisema Serikali inatambua uwepo wao wa kimasomo nchini Cuba na
kwamba inatarajia kupata mchango mkubwa kutoka kwao punde wamalizapo masomo
yao.
“Nawaomba msome kwa bidii
na mfaulu mitihani yenu. Elimu yenu iwasaidie katika ajira na muweze kurejesha
mikopo mliyopewa na Serikali ili iwanufaishe wengine.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka Mabalozi wote
wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuhakikisha wanatangaza
vivutio vya utalii.
Alisema Tanzania imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii,
hivyo ni vema Mabalozi wakavitangaza jambo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya
watalii wanaokuja nchini.
Miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyoko nchini ni pamoja na
mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar, mbuga mbalimbali zenye wanyama wa aina
tofauti tofauti.
Awali Mwenyekiti wa wanafunzi hao, Bw. Goodchance
Tarimo alimuhakikishia
Waziri Mkuu kwamba watarejea nyumbani mara baada ya kumaliza masomo yao nchini
humo.
Alisema wao wanaimani kubwa na Serikali na wanaunga
mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa Taifa kwa lengo la kuboresha
maendeleo pamoja na kukuza uchumi.
“Tunapongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano
katika kujenga uchumi wa viwanda,
mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ujenzi wa miundombinu ya kisasa.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 21, 2017.
No comments:
Post a Comment