WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua miongozo ya
Kitaifa ya Kusimamia Mafunzo ya Vitendo kwa Wahitimu (Internship Guidelines) na Mafunzo ya
Uanagenzi (Apprenticeship Guidelines) mahala pa kazi, leo (Jumamosi, Septemba
16) mjini Dodoma.
Amesema miongozo hiyo inalenga kuongeza
ari kwa waajiri na wadau wengine kushiriki katika kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi za
kazi ili kuhakikisha wahitimu na wanagenzi wanapata stadi za kazi na ujuzi stahiki wa kuajirika au
kujiajiri.
Waziri Mkuu amesema miongozo hiyo
ambayo inakwenda kuboresha mafunzo ya uanagenzi na kwa wahitimu itachochea
ukuzaji wa viwanda na kupunguza ukosefu wa ajira kwa watanzania hususan vijana.
Amesema Serikali imekua ikipokea
malalamiko kutoka kwa waajiri kwamba wahitimu wengi wa ngazi mbalimbali za
mafunzo wanaingia katika soko la ajira wakiwa hawana ujuzi unaohitajika na
hivyo waajiri kulazimika kutafuta wafanyakazi kutoka nje ya nchi.
Amesema baada ya kupokea malalamiko
hayo Serikali, Waajiri na Wafanyakazi na walikubaliana kuimarisha mfumo wa utoaji
mafunzo yanayofanyika maeneo ya kazi ili kuhakikisha mafunzo yatolewayo maeneo
ya kazi yana ubora unaohitajika.
“Kuimarisha uwezo wa nguvu kazi ya
Taifa ni muhimu na njia bora ni kuboresha utoaji mafunzo kwa vitendo mahali pa
kazi kwa kuweka miongozo bora itakayowaongoza wadau wote wakiwemo Serikali, Waajiri,
Wafanyakazi na Vijana kutoa Mafunzo.”
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Magufuli
alipoanza kuweka malengo ya ujenzi wa viwanda, mbali na kuwezesha kukua kwa
kilimo na kuongeza thamani mazao, pia alilenga kupanua wigo wa ajira za
viwandani ambapo kiwanda kinaweza kuajiri watu zaidi ya 1000.
Amesema miongozo hiyo itasaidia
kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kuhakikisha Taifa linakuwa na nguvu
kazi yenye weledi wa kutosheleza mahitaji ya soko la ajira na kuvutia
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa
upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama amesema miongozo hiyo
inaweka mfumo madhubuti wa kuandaa, kutekeleza, kusimamia, kuratibu na
kufuatilia mafunzo husika mahala pa kazi.
Pia miongozo hiyo inabainisha
majukumu ya wadau muhimu wa mafunzo hayo ambayo ni pamoja na kuweka bayana utaratibu
wa kugharamia mafunzo ikiwa ni pamoja na kushirikisha Serikali, waajiri na
wazazi.
“Miongozo imebainisha majukumu ya
wadau katika kutoa mafunzo ambao ni Serikali, waajiri, taasisi za mafunzo,
taasisi za mitaala na wanagenzi na wahitimu. Pia imebainisha vigezo vya
kuwapata washiriki wa mafunzo na muda wa mafunzo.”
Pia miongozo hiyo imebainisha mfumo
wa kitaasisi wa kuratibu na kuhakikisha ubora wa mafunzo kwa kuunda kamati ya
Utatu wa Taifa ya kuratibu, kufuatilia tathmini ya mafunzo chini ya usimamizi
wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMAMOSI, SEPTEMBA 16, 2017
No comments:
Post a Comment