Na Mwandishi Wetu
VYAMA vya Riadha vya Mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani vimetakiwa kuthibitishwa haraka iwezekanavyo ushiriki wao katika mashindano maalumu ya wanawake yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 25 na 26 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Riadha
Tanzania (RT), Ombeni Zavalla, mashindano hayo yanayofanyika kwa udhamini wa
Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA), yatashirikisha wasichana
chini ya miaka 20.
Zavalla, alisema mashindano hayo yanalenga kuibua vipaji na
kuhamasisha wanawake kujikita katika mchezo huo kama ilivyokuwa zamani wakati
wakifanya vema kitaifa na kimataifa.
Katibu Msaidizi huyo, alisema vyama vya mikoa yote
vimekwishapewa taarifa rasmi isipokuwa mikoa sita pekee, hivyo wanapaswa
kuwasiliana na RT kuthibitisha ushiriki wao haraka iwezekanavyo ili mipango ya
maandalizi iendelee bila vikwazo.
“Vyama vya mikoa tayari tumewatumia taarifa rasmi, hivyo
wanapaswa kuchagua wachezaji wao wa kuunda timu zao za mikoa na kuanza
maandalizi ili kuja kutoa ushindani, lakini kikubwa ni kuwasiliana nasi mara
moja kututhibitishia ushiriki wao ili tuendelee na mipango ya maandalizi bila
kikwazo,” alisema Zavalla.
Katibu huyo msaidizi, alifafanua kuwa kila mkoa unapaswa kuwa
na wachezaji watano na kiongozi mmoja, ikiwezekana naye awe mwanamke.
Alisema mikoa itapaswa kugharamia timu zao hadi jijini Dar es
Salaam na wakifika gharama zote za malazi na usafiri wa ndani zitagharamiwa na
JICA.
Aliitaja mikoa ambayo imepewa taarifa rasmi ni mikoa mitano
ya Zanzibar kupitia Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA).
Aliitaja mikoa hiyo ni Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja,
Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kuzini Pemba.
Kwa bara ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida,
Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga,
Iringa, Mbeya, Njombe, Mtwara, Kigoma, Lindi na Ruvuma.
Mikoa ambayo vyama vyao ya mikoa haviko hai lakini wamepewa
taarifa kupitia Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS), ni Geita, Rukwa, Katavi, Geita
na Songwe.
Katibu huyo msaidizi, alitoa wito
kwa wadau mbalimbali mikoani kushirikiana na vyama hivyo ili kuhakikisha
wanawawezesha wanawake kushiriki mashindano hayo hasa ukizingatia medali ya
kwanza katika mchezo wa riadha hapa nchini ililetwa na Mwanamke, Theresia
Dismas mwaka 1964.
No comments:
Post a Comment