HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 16, 2017

Waegesha ndege wa JNIA wapigwa msasa


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama kulia) jana akifungua mafunzo ya wiki moja ya Waegesha ndege yanayofanyika kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kinachomilikiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (CATS) kilichopo kwenye Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (TBI).
Wakufunzi Ralf Overduya (kushoto) na Martiyn Ouwendyki kutoka Kiwanja cha Ndege cha Hague cha Uholanzi jana wakianza kufundisha baadhi ya waegesha ndege wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) katika mafunzo yanayofanyika kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kinachomilikiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki, wakufunzi na waandaaji wa mafunzo ya waegesha ndege yaliyoanza jana kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Avi Assist wa Uholanzi Bw. Tom Kok.


Na Mwandishi Wetu

WAEGESHA ndege 10 wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), jana walianza mafunzo ya siku saba ya uegeshaji ndege kutoka kwa wakufunzi wa Kiwanja cha Ndege cha Hague cha Uholanzi yanayofanyika katika Chuo cha Usafiri wa Anga (CATS) jijini Dar es Salaam.

Akifungua mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatazidi kuwajengea uwezo na uzoefu washiriki hao.

Bw. Mayongela amewasisitiza washiriki hao kuzingatia kila wanachofundishwa ili waweze kuwa mahiri na weledi katika uongozaji wa ndege za ndani na nje ya nchi zinazotumia kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

“Waongoza ndege ni moja ya kazi inayohusisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya watoa huduma ndani ya kiwanja cha ndege, hivyo ni lazima tufikie viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria kimataifa,” amesema Bw. Mayongela.

Hata hivyo, amesema TAA inajukumu kubwa la kuwaongezea uwezo watumishi wake kwa kuwapeleka kwenye mafunzo mbalimbali ili kujijengea uwezo na maarifa.

Bw. Mayongela amewashukuru waendeshaji wa mafunzo hayo yanayotolewa na mfuko wa Avi Assist wa Uholanzi, ambapo amewahahakikishia kuendeleza ushirikiano waliouanzisha kwa kushirikiana katika utoaji wa mafunzo ya kada mbalimbali.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Waongoza ndege cha JNIA, Bw. Lugano Mwinuka amesema mafunzo haya yamekuja wakati muafaka, kwa kuwa walikuwa yakiyahitaji kwa muda mrefu, na sasa anauhakika wa washiriki wataongeza ujuzi katika utendaji wao wa kazi.

Bw. Mwinuka amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa nadharia na vitendo, ambapo washiriki hao wamegawanywa katika makundi mawili ya watu watano, ambao ni Earisner Waihula, Emmanuel Nyaulingo, Anunciatus Alex, Fadhili Meena na Oscar Kibiki.

Watakaoingia kundi la pili ni pamoja na Denis Kinyaga, Zennobius Mwimba, Raynard Komba, Said Mussa na Meshack Elisante.

No comments:

Post a Comment

Pages