Na
Mwandishi Wetu- Tarime, Mara
Serikali kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo ya watoto wa kike hapa nchini wameendesha
mafunzo kwa waendesha bodaboda walioko
wilaya ya Tarime mkoani Mara kuwahamasisha
vijana hao kuunga mkono juhudi za
kitaifa za kutokomeza mimba za utotoni kwa wasichana walioko shule ya msingi na
sekondari.
Akieleza malengo ya
mafunzo hayo, Afisa Mkuu wa Maendeleo ya Jamii Bibi Anna Shengweli amebainisha kuwa
madreva wa bodaboda ni kundi mahususi katika ulinzi wa watoto wa kike kwani kutokana
na shughuli zao wanakutana mara nyingi na watoto wa kike wakiwa katika
mazingira hatarishi.
“Wakiwa katika kazi zao
za kila siku bodaboda na wanapishana na watoto wa kike wakitekeleza majukumu
yao mbalimbali ikiwemo kwenda na kurudi kutoka shule, kuteka maji visimani,
kuchunga mifugo porini, sokoni, stendi ya basi na kadhalika’’ alisema Bibi Anna.
Kwa upande wake
mwezeshaji kutoka ‘Shirika la Save the Childern’ Bw. John Komba amesema kuwa ni muhimu kuwajengea uelewa
waendesha bodaboda ili wawe tayari kutambua na kutekeleza wajibu wa kuwaelimisha
na kuwalinda watoto wa kike waepukane na vitendo vya ngono wawapo nyumbani,
shuleni, njiani, sokoni, mitaani, na katika shughuli za kijamii kwa ujumla.
“Mafunzo haya
yatawasidia waendesha bodaboda kuwa mabalozi wa usalama na ulinzi wa mtoto wa
kike ili kupunguza idadi ya wasichana wanaoacha shule kutokana na changamoto ya
mimba za utotoni na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao, pamoja na kuwashirikisha
katika mtandao wa usalama wa mtoto katika ngazi ya kata na mitaa. Juhudi hizi
zikifanyika zitachangia kupunguza tatizo la mimba za utotoni kutoka asilimia 27
hadi asilimia 8 ifikapo mwaka 2022 alisema Bw. Komba.
Naye Mkurugenzi Mkazi
Shirika la REPPSI Bibi. Edwick Mapalala amefafanua kuwa mafunzo haya yatasaidia
kumwezesha mtoto wa kike aweze kuwa na maisha bora yenye usalama maana
atahakikishiwa ulinzi na ndugu wa karibu katika familia, watoa huduma
wanaomzunguka mtoto, na jamii yote kwa ujumla.
“Mafunzo haya
yataimarisha uaminifu wa madreva wa bodaboda kuzingatia umuhimu wa kuzuia na
kupunguza matukio ya mimba za utotoni kwa watoto wa kike” alisema Bibi Edwick.
Aidha Mwenyekiti wa
madreva bodaboda wilayani Tarime Bw. Paschal Joseph, ameishukuru Serikali kwa
kuandaa mafunzo hayo pamoja na wadau mbalimbali na ameahidi kuwaheshimu,
kuwalinda na kuwapa haki sawa watoto wa kike katika ngazi ya familia na jamii
kwa ujumla.
Semina hiyo ya siku
moja iliyoandaliwa na mashirika yautetezi
haki za watoto nchini wakiwemo UNICEF, Save the Children, Plan
International Tanzania, REPSSI na CDF na
jumla ya washiriki 40 wamehudhuria mafunzo hayo kati ya vijana 1600
wanaojihusisha na uendeshaji wa Bodaboda
wilayani Tarime.
Mafunzo hayo
yamefanyika ikiwa ni moja kati ya shughuli muhimu za maadhimisho ya Siku ya
Kimataifa ya Mtoto wa Kike 2017 yenye kauli mbiu inayosema “Tukomeza Mimba za Utotoni Tufikie
Uchumi wa Viwanda’.
No comments:
Post a Comment