Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA),
Bi. Edda Sanga (kushoto) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani)
katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Wahanga wa Ajali za
Barabarani. Kulia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Walemavu Tanzania
(SHIVYAWATA), Felician Mkude.
Dar es Salaam, Tanzania
MTANDAO
wa wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera
ihusuyo usalama barabarani umeiomba Serikali kuifanyia maboresho sheria
ya Usalama barabarabi ya mwaka 1973 ili iweze kukabiliana ipasavyo na
suala la ajali za barabarani pamoja na athari zinazotokana na ajali
hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
(TAMWA), Bi. Edda Sanga alipokuwa akisoma tamko la pamoja la asasi hizo
katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Wahanga wa Ajali za
Barabarani.
“Pamoja na mambo mengine, katika
kuadhimisha siku hii tunaisihi serikali na watunga sheria kuifanyia
maboresho sheria ya Usalama barabarabi ya mwaka 1973 ili iweze
kukabiliana ipasavyo na suala la ajali za barabarani pamoja na athari
zinazotokana na ajali hizo,” alisema Bi. Sanga.
Alisema
miongoni mwa maeneo wanaoshauri marekebisho/maboresho ni pamoja na
matumizi ya mikanda, ambapo Sheria ya sasa ya Usalama barabarani inasema
ni kosa kisheria kwa dereva na abiria anayekaa kiti cha mbele
kutokufunga mkanda wakati wa safari lakini sheria haisemi chochote kwa
abiria wanaokaa viti vya nyuma.
Alisema licha
ya Kanuni za SUMATRA zinamtaka abiria yeyote kufunga mkanda ila kwa vile
sheria mama (Road Traffic Act of 1973) ipo kimya katika eneo hilo
utekelezaji wa kanuni hii unakuwa mgumu.
Alisema
eneo linguine ni pamoja na matumizi sahihi ya kofia ngumu, kwani Sheria
ya sasa ya usalama barabarani inatambua kosa kwa mwendesha pikipiki
kutokuvaa kofia ngumu lakini sheria hiyo haisemi chochote kwa abiria
anayepanda katika chombo hicho wala kutaja aina na ubora wa kofia
inayofaa.
“Kwa matumizi ya vilevi na uendeshaji
vyombo vya usafiri: Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa
itakuwa kosa kwa mtu yoyote kuendesha chombo cha moto akiwa na kiwango
cha kilevi katika damu yake kinachozidi asilimia 0.08% katika mfumo wa
mwili.
Kiwango hiki ni kikubwa sana
kikilinganishwa na tafiti zilizofanywa na Shirika la afya duniani na
kupendekeza kiwango asilimia 0.05% kwa dereva aliyebobea na asilimia
0.02% kwa dereva mchanga. Hivyo basi ni rai yetu kuwa sheria ifanyiwe
marekebisho ili iendane na kiwango cha sasa cha kimataifa kilichofanyiwa
utafiti,” alisisitiza Bi. Sanga.
Aidha
aliongeza kuwa adhabu zinazotolewa kwa sasa hazikidhi wala kuleta hofu
kwa maderava wasiotaka kutii sheria na kanuni hivyo kuendelea kufifisha
juhudi za kudhibiti tatizo la ajali za barabarani.
“Mwendokasi
umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazogharimu uhai wa watu wengi.
Sheria yetu inayo mapungufu kadhaa pamoja na juhudi nyingi za Jeshi la
Polisi na wadau wengine kutaka kudhibiti jambo hili lemeendelea kuwa
tatizo. Mfano Sheria ya usalama barabarani ya 1973 Kifungu cha 51(8)
inatambua maeneo machache katika kuzuia mwendokasi, ni muhimu Sheria
sasa itamke maeneo yote na si yale ya mjini tu au makazi, itamke wazi
kuhusu maeneo ya shule, nyumba za ibada, maeneo ya michezo na mbuga za
wanyama,” aliongeza Bi. Sanga katika taarifa hiyo.
Pamoja
na mambo mengine, alisema sheria ya sasa ipo kimya juu ya suala la
vizuizi vya watoto katika vyombo vya moto hasa kwa magari binafsi na
tumeendelea kushuhudia madhara makubwa katika ajali zilizohusisha watoto
vikiwemo vifo.
Hata hivyo mtandao huo
umewasihi wananchi kuwa na taadhari pindi watumiapo vyombo vya moto
bila kujali mapungufu yaliyopo kwenye sheria za usalama barabarani ili
kupunguza matukio ya ajali.
Kwa upande wake,
Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) usalama barabarani Mary
Kessy, akitoa ufafanuzi kwa wanahabari, alibainisha takwimu zinaonyesha
takribani watu milioni 1.25 duniani hufariki kila mwaka; huku nchini
Tanzania asilimia 76 ya ajali za barabarani husababishwa na uzembe wa
madereva, asilimia 8 ubovu wa barabara na ubovu wa vyombo vya moto
kuchangia ajali hizo kwa asilimia 16.
Kauli
mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Ifikapo 2020: Kupunguza vifo na
ajali za barabarani kwa asilimia 50%”. Mtandao wa Wadau kutoka asasi za
kiraia unaotetea marekebisho ya Sheria za Sera zihusuyo usalama
barabarani Tanzania unaundwa na asasi zifuatazo;- TAWLA, TAMWA, WLAC,
TCRF, TLS, TMF, RSA, AMEND TANZANIA, SHIVYAWATA, TABOA pamoja na SAFE
SPEED FOUNDATION.
No comments:
Post a Comment