Askari Polisi wakishirikiana na ndugu wa Mwanafunzi aliyepotea Humphrey Makundi wakifukua Kaburi ulimozikwa mwili wa mtu aliyeokotwa Mto Ghona katika wilaya ya Moshi.
Baba mzazi wa Mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Scolastica aliyepotea,Jackson Makundi (Katkati) akijadili jambo na wanandugu wakati zoezi la kufukua kaburi likiendelea.
Baba mzazi wa Mwanafunzi Humphrey, Jackson Makundi (Mwenye suti nyeupe) akitizama mwili (haupo pichani) baada ya kaburi kufukuliwa.
Askari Polisi na Wanandugu wa kijana aliyepotea wakijaribu kusaidia kumnyanyua mzazi wa Mwanafunzi huyo kutoka katika eneo lilipo kaburi lililofukuliwa .
Baba mzazi wa Mwanafunzi Humphrey, Jackson Makundi (Mwenye suti nyeupe) akisindikizwa kutoka katika eneo la Makaburi ya Karanga katika manispaa ya Moshi.
Mwili uliofukulia katika Makaburi hayo ukiwekwa katika gari la Polisi kwa ajili ya kwenda kuhifadhiwa katika Hosptali ya Rufaa ya KCMC.
Gari la Polisi likiwa na mwili uliofukuliwa katika Makaburi ya Karanga.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini
UTATA umeighubika familia ya Jackson Makundi ambayo kijana wake
aliyetambulika kwa jina la Humphrey Makundi,Mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya
Scolastica iliyopo mji mdogo wa Himo kupotea katika mazingira tatanishi.
Utata wa kupotea kwa mwanafunzi huyo unatiliwa shaka zaidi na
familia hiyo baada ya kufukuliwa kwa kaburi ulimozikwa mwili uliookotwa mto
Ghona mita 300 ,jirani na shule hiyo ukidaiwa kushabihiana na wa mwanafunzi
huyo
Humphrey Makundi, mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya
sekondari ya Scolastica anatajwa kupotea tangu Novemba 7 mwaka huu akiwa
shuleni hapo huku wanafunzi wenzake wakiendelea na mitihani ya kidato cha Pili
ya upimaji ya kitaifa .
Familia ya kijana huyo yenye makazi yake mkoani Dodoma
ikalazimika kutumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa za kupotea kwake ikidai
mazingira ya kutoweka kwake ni ya kutatanisha na baadae kuwasilisha taarifa
katika kituo cha Polisi cha Himo .
Kutokana na kuwepo kwa taarifa za kuokotwa kwa mwili huo
,familia iliwasilisha maombi katika mahakama ya Hakimu Mkazi, Moshi na mahakama
ikaamuru kufukuliwa kwa Kaburi hilo zoezi lililoanza majira ya saa 8:30 mchana
na kudumu kwa zaidi ya saa moja.
Jeshi la Polisi liliongoza zoezi hilo katika makaburi ya Karanga
huku likishuhudiwa na ndugu wa mtoto aliyepotea ambapo baada ya mwili kutolewa
kaburini hali ya simanzi ilionekana katika nyuso za baadhi ya ndugu wa
Mwanafunzi huyo akiwemo baba mzazi wa kijana huyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro,Kamishna Msaidizi wa
Polisi ,Hamis Issa akathibitisha uwepo wa tukio hilo huku akieleza kuwa tayari
jeshi la Polisi linawashikilia wati 11 akiwemo mmiliki wa shule hiyo Edward
Shayo huku likifanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo mawili.
Mwili uliofukuliwa katika makaburi ya Karanga upande wa marehemu
wasiokuwa na ndugu ulipelekewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC kwa
uchunguzi zaidi chini ya uangalizi wa jeshi la Polisi wakishirikiana na
madaktari kutoka KCMC.
No comments:
Post a Comment