Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Burundi na Msumbuji, Bi Bella Bird, wakisaini Mkataba wa Mkopo wenye masharti nafuu wa Sh. Dola za Marekani milioni 150 sawa na Shilingi bilioni 340 kwa ajili ya Mradi wa kuibua fursa za Utalii Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi, Msumbiji na Burundi Bi. Bella Bird (kushoto) wakibadilishana Mkataba wa Mkopo wenye masharti nafuu wa Sh. bilioni 340 kwa ajili ya Mradi wa kuibua fursa za Utalii katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Benny Mwaipaja, Dar
es Salaam
BENKI ya Dunia imeipatia
Tanzania Mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 150, sawa na
takriban Shilingi bilioni 340 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kufungua
fursa za utalii katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania.
Mkataba wa mkopo huo
umetiwa saini Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia anayehudumia nchi
za Tanzania, Malawi, Msumbiji na Burundi, Bi. Bella Bird.
Bw. James alisema
kuwa mkopo huo umelenga kuimarisha miundombinu ya utalii katika ukanda huo wa
kusini ikiwemo ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege, madaraja pamoja na kuibua
fursa nyingi za utalii ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Alisema pia kwamba mradi
huo umelenga kuwajengea uwezo wananchi wanaozunguka maeneo ya utalii kwa
kuanzisha miradi itakayo chochea maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi pamoja na
kuendeleza uhifadhi katika maeneo yao.
Aidha, mkopo huo
utatumika katika kampeni ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko katika
ukanda huo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ili kuvutia watalii wengi zaidi
kutembelea maeneo hayo badala ya hali ilivyo sasa ambapo watalii wengi
wanatembelea vivutio vilivyoko ukanda wa Kaskazini.
Mradi huo
utakaotekelezwa kwa kiasi kikubwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa
Tanzania-TANAPA, utainufaisha zaidi Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mikumi, Udzungwa
na Pori la Akiba na Selous.
Alisema kuwa manufaa
hayo yatalenga kujengwa viwanja vya ndege, barabara hifadhini, utunzaji wa
mazingira utakao uwezesha mto Ruaha Mkuu kutiririsha maji muda wote katika Hifadhi
ya Taifa ya Ruaha kupitia uwanda wa Usangu.
“Mpango wa kuibua
fursa za utalii katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania, umelenga kuimarisha
usafiri wa anga na nchi kavu ambapo uwanja mkubwa na wa kisasa utajengwa mkoani
Iringa pamoja na kuboresha barabara inayotoka Iringa hadi Msembe yenye urefu wa
kilometa 105” alisema Bw. James
Aisema kuwa hatua
hiyo inatarajia kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi na kupunguza
gharama za usafiri kutoka katika maeneo ya Zanzibar, Dar es Salaam na
Kilimanjaro hivyo kuongeza mapato ya Serikali.
Bw. Doto James aliishukuru
Benki ya Dunia kwa mkopo huo utakao changia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa
nchi na maendeleo ya wananchi wake kupitia sekta ya utalii.
Kwa upande wake
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali, Gaudence Milanzi
alisema kuwa mradi huo, utahusisha ujenzi wa viwanja 15 vya ndege, ujenzi wa
kilometa 982 za barabara kwenye hifadhi, kununua mitambo ya kukarabati
barabara, kuimarisha reli ya TAZARA ili kuwawezesha watalii kufika kwenye Pori
la Akiba la Selous.
Aidha, alisema kuwa
wananchi wanaozunguka eneo la mradi watapatiwa mafunzo ya namna ya kuongoza
watalii, kutoa huduma kwenye hoteli na kuwajengea uwezo wa kutengeneza bidhaa
zinazohusiana na utalii ili wajiongezee kipato.
Meja Jenerali Milanzi
alisema kuwa wanategemea mradi huo utaongeza idadi ya watalii kutoka milioni
moja hivi sasa hadi kufikia zaidi ya watalii milioni 2 ifikapo mwaka 2020.
Akizunguza wakati wa
tukio hilo, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, hapa nchini Bi. Bella Bird
alisema kuwa mkopo huo ulioridhiwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Jijini
Washington DC Septemba 28, 2017, umelenga kukuza uchumi wa Tanzania kupitia
sekta hiyo ya utalii na kupunguzia umasikini wananchi wake.
“Utalii na uhifadhi
vinakwenda pamoja na kwamba vitu hivyo viwili vitaisaidia nchi kukua kiuchumi
na kukuza ajira ya watu wake kwa kiwango kikubwa hivyo kuondokana na umasikini
ikichagizwa pia na kilimo” alisisitiza Bi. Bella Bird.
Alisema sekta ya
utalii inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya watu na wanyama,
ujangili, na ndiyo maana Benki ya Dunia imeamua kuisaidia Serikali na taasisi
zinazojihusha na kudhibiti changamoto hiyo kwa kuzijengea uwezo wa kukabiliana
nazo.
Bi. Bird alisema kuwa
mradi huo utakuja na suluhisho la changamoto ya wananchi kuwa sehemu ya
uhifadhi kwa kuwapa miradi ya maendeleo itakayokuwa mbadala wa shughuli
walizokuwa wakifanya kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo kuanzisha utalii wa
kiutamaduni, kilimo ili waendeleze maisha yao.
No comments:
Post a Comment