HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 18, 2017

MAJALIWA:MWENENDO WA UKUAJI UCHUMI WA TAIFA UNARIDHISHA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa Taifa unaridhisha, ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 17, 2017) wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge, mjini Dodoma.

“Mwenendo wa uchumi wetu ni wa kuridhisha, mfano, ukuaji wa uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7, robo ya pili ilikuwa asilimia 7.8 na nusu ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa ni asilimia 6.8.”

Amesema hali hiyo inafuatia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na usimamizi thabiti wa matumizi ya Serikali, ambapo nakisi ya bajeti ya Serikali imeshuka na kufikia asilimia 1.9 kwa mwaka 2016/2017

Pia amesema akiba ya fedha za kigeni inatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa zaidi ya kipindi cha miezi mitano, ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne.

Akizungumzia kuhusu kasi ya upandaji bei, Waziri Mkuu amesema takwimu zinaonyesha kwamba katika nusu ya mwaka 2017, mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika kiwango cha tarakimu moja. 

“Takwimu zinaonyesha kwamba mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Oktoba 2017 ulikuwa ni asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilima 5.3 mwezi Septemba, 2017.”

Amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa bei wa bidhaa za vyakula, ambavyo vimepungua kutoka wastani wa asilimia 9.3 mwezi Septemba, 2017 hadi asilimia 8.8 mwezi Oktoba, 2017.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii ianzishe Mamlaka ya Fukwe za Bahari na Maziwa ili kutangaza na kuendeleza fukwe ambazo hazina shughuli.

Amesema fukwe za bahari ni eneo mojawapo ambalo likiendelezwa vizuri, linaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi, hivyo ni lazima zipewe kipaumbele.

Pia ametoa wito kwa wizara hiyo iongeze kasi ya kuleta mabadiliko katika sekta nzima ya maliasili ili iweze kuchangia zaidi kwenye uchumi. 

Ametolea mfano Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo imefanikiwa kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 60.1 mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi bilioni 102 mwaka 2016/2017.

Waziri Mkuu amesema ongezeko hilo la mapato limekuja baada ya Serikali kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia njia ya kielektroniki.
 

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, NOVEMBA 17, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages