HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 22, 2017

WRATZ WAITAKA SERIKALI KUPELEKA WAKUNGA WENYE WELEDI VIJIJINI

NA JANETH JOVIN

MUUNGANO wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama (WRATZ), umeitaka serikali kupeleka wakunga na wauguzi wa kutosha wenye ujuzi na weledi katika vituo vya afya vilivyopo nchini, hasa maeneo ya vijijini ili kuweza kupunguza vifo vya kinamama 30 vinavyotokea kila siku wakati wanapojifungua.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mratibu wa Taifa wa Utepe huo, Rose Mlay wakati wa Mkutano uliyowakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya afya ili kujadili takwimu za afya ya mama na mtoto na njia za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga vitokanavyo na uzazi.

Mlay alisema takwimu za afya mwaka 2015/16 zilizotolewa na Taasisi ya Takwimu nchini zimeonyesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi zimeongezeka kutoka 24 kwa siku hadi kufikia 30 idadi ambayo ni mbaya na inapaswa kupunguzwa.

Alisema ili kupunguza vifo hivyo serikali inatakiwa kuwa na wakunga na wauunguzi wa kutosha wenye stadi katika vituo vya afya na kuongeza kuwa kuzuia vifo hivyo vya wajawazito na watoto wachanga kutaliinua taifa kufikia malengo ya millennia.

"Kupitia mkutano huu wadau kwa pamoja tumekutana na tumejadili hizi Takwimu za Afya ya mama na mtoto kwa kina na kuweka baadhi ya mikakati ambayo tunaamini kama itafuatwa vizuri badi tunaweza kupunguza tatizo hili,” alisema Mlay

Aidha ameishauri jamii kuwa mstari wa mbele katika kuzuia vifo hivyo vitokanavyo na uzazi kwa kuhakikiasha mama mjamzito anajifungulia katika kituo cha Afya.

Alisema jamii ikiwa na utararibu wa kumpeleka mama mjamzito katika kituo cha Afya inaweza kusaidia kupunguza na kumalizika kabisa kwa tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi.

“Kupoteza mtoto na mama ni ajali mbaya ambayo imekuwa ikitokana nchini kwetu sasa ili kuweza kupunguza ajali hiyo inatubidi kila mtu abadilike kwa Serikali ihakikishe inakuwa na wataalamu wa kutosha na kwa wanawake wenyewe wahakikishe wanajifungulia hospitali na sio nyumbani,” alisema.

Naye Msajili wa Baraza la Wauguzi na Ukunga Tanzania, Lena Mfalila alisema umefika wakati wakuwasomesha wakunga na wauguzi wengi zaidi kisha kuwapeleka hata wawili katika kila kituo cha kutolea huduma za afya hasa vilivyopo vijijini.

No comments:

Post a Comment

Pages