HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 15, 2017

LAPF YANGA’RA UANDAAJI WA HESABU KWA MIAKA 7 MFULULIZO

Na Mwandishi Wetu

Mfuko wa Pensheni wa LAPF umepata tuzo ya uandaaji bora wa hesabu katika sekta ya Hifadhi ya Jamii na Bima kwa mwaka 2015/16 inayotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu (NBAA).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mjini Dodoma kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Eliud Sanga, Mkurugenzi wa fedha wa Mfuko huo Bw. John Kida amesema kuwa mfuko huo umepata tuzo hiyo kwa miaka saba mfululizo ikiwa ni ishara ya utendaji mzuri na wenye kuchochea ukuaji wa Mfuko na maendeleo ya Taifa kwa ujumla kutokana na uwekezaji unaofanywa katika sekta mbalimbali.

“Kwa mwaka 2015/2016 mapato yanayotokana na uwekezaji katika vitega uchumi yalifikia shilingi bilioni 96.03 ikilinganishwa na shilingi bilioni 72.72 kwa mwaka 2014/2015 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 32.” Alisisitiza Kida

Akifafanua Kida amesema kuwa mafanikio ya mfuko huo yanatokana na kuongezeka kwa wanachama ambao hadi Septemba 2017 walikuwa wamefikia 180,401.

Aliongeza kuwa Mfuko huo katika kipindi cha mwaka 2015/2016 umelipa mafao kwa wanachama 8,011 ambapo jumla ya shilingi bilioni 107.24 zililipwa kama mafao kwa wanachama.

Akieleza mafanikio mengine Kida amesema kuwa michango ya wanachama imeongezeka ambapo kwa mwaka 2015/2016 imefikia shilingi bilioni 279.68 ikilinganishwa na shilingi bilioni 210.07 sawa na ongezeko la asilimia 33 hali iliyosababishwa na kuoongezeka kwa wanachama kutoka 150,835 hadi kufikia wanachama 166,260 mwezi June 2016.

Kwa upande wake Meneja Masoko na Uhusiano wa Mfuko huo Bw. James Mlowe amesema mafanikio ya mfuko huo yanatokana na utendaji makini unaozingatia utawala Bora katika kusimamia rasilimali za Mfuko huo ikiwemo fedha.

Mfuko wa Pensheni wa LAPF umewekeza katika vitega uchumi mbalimbali ambapo hadi kufikia June 2016 ulikuwa umewekeza jumla ya shilingi trilioni 1.09, wakati kwa kipindi cha mwezi June 2015 mfuko huo uliwekeza bilioni 884.26 katika vitega uchumi mbalimbali kama dhamana za Serikali, Amana za mabenki, majengo, hisa za makampuni na uwekezaji katika Kampuni tanzu.
 PIX 1. Mkurugenzi wa Fedha wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF Bw. John Kida akizungumza na waandishi kuhusu mfuko huo kupata tuzo ya uandaaji bora wa hesabu katika sekta ya hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya kwa mwaka 2015/2016 ambapo Mfuko huo umeshika nafasi ya kwanza,  Tuzo hiyo imetolewa na  Bodi ya Taifa ya Uhasibu (NBAA) hivi karibuni. Kulia ni Meneja Masoko na Uhusiano wa LAPF Bw. James  Mlowe.
  Meneja Masoko na Uhusiano wa LAPF Bw. James Mlowe akieleza mikakati  iliyouwezesha mfuko huo kupata tuzo hiyo ikiwemo uwajibikaji na utawala bora katika kusimamia rasilimali fedha katika mfuko huo. Kushoto ni   Mkurugenzi wa Fedha wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF Bw. John Kida.
Meneja Masoko na Uhusiano wa Mfuko wa Pensheni wa  LAPF  Bw. James  Mlowe akifurahia tuzo ya uandaaji bora wa hesabu katika sekta ya hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya kwa mwaka 2015/2016 ambapo Mfuko huo umeshika nafasi ya kwanza,  Tuzo hiyo inatolewa na  Bodi ya Taifa ya Uhasibu (NBAA) hivi karibuni.
Meneja Matekelezo wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF  Bw. Victor Kikoti, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mafao yanayotolewa na mfuko huo na faida wanazopata wananchi kutokana na mafao hayo .
 Mkurugenzi wa Fedha wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF  Bw. John Kida  (katikati) akionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) tuzo ya uandaaji bora wa hesabu katika sekta ya hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya kwa mwaka 2015/2016 ambapo Mfuko huo umeshika nafasi ya kwanza, Tuzo hiyo imetolewa na  Bodi ya Taifa ya Uhasibu (NBAA) hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Pages