Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa
(BMT), Mohamed Kiganja (kulia) akimpongeza Alex Temba mara baada ya uchaguzi wa
Shirikisho la Michezo la Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI), uliofanyika hivi
karibuni kwenye hoteli ya Mount Uluguru mkoani Morogoro.
Uongozi mpya wa Shirikisho la Michezo la Idara
na Wizara za Serikali (SHIMIWI), mara baada ya kutangazwa na msimamizi wa
uchaguzi uliofanyika hivi karibuni kwenye hoteli ya Mount Uluguru mkoani
Morogoro.
Na Mwandishi Wetu
MWEKA Hazina, William Mkombozi ‘Mgosi’ amerudi kwa kishindo
katika nafasi hiyo baada ya kushinda kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Michezo
kwa Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI), uliofanyika hivi karibuni kwenye
ukumbi wa hoteli ya Mount Uluguru mkoani Morogoro.
Mkombozi aliyewahi kuongoza katika miaka ya mwanzoni ya 2000
akiwa na aliyewahi kuwa mjumbe na baadaye Katibu Mkuu, Bw. Ramadhani Sululu, lakini
baadaye alikaa pembeni sasa amechaguliwa tena kwa kura 23.
Naye Alex Temba aliyeongoza kwa muda mrefu katika Klabu
yenye wachezaji mahiri ya Uchukuzi, alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi baada ya
kushinda kwa kura 28 na kumbwaga Margreth Mtaki aliyepata kura 15.
Hatahivyo, nafasi ya Mwenyekiti ilirudi tena kwa Daniel
Mwalusamba aliyekuwa hana mpinzani kwa kupata kura 42; huku Ally Katembo akichaguliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti kwa kura 41; wakati Moshi Makuka ametetea nafasi yake ya Ukatibu kwa
kura 38 dhidi ya Andrew Sekimweri aliyeondoka na kura sita.
Katika nafasi ya Mweka Hazina Msaidizi, ameshinda Frank
Kibona kwa kura 21; wakati walioshinda kwenye ujumbe wa kamati ya utendaji na
kura zao zikiwa kwenye mabano ni Apolo Kayungi (44), Assumpta Mwilanga (42),
Aloyce Ngonyani (40), Damiani Manembe (39) na Seleman Kifyoga (31).
Kwa upande wa nafasi ya viti maalum wanawake walioshinda ni Mwajuma
Kisengo (20) na Mariam Kihange (18) na waliwashindwa ni Costance Momadi (16) na
Buya Masunga (12).
Michezo ya SHIMIWI inayoshirikisha watumishi wa umma
imepoteza mvuto kwa kutofanyika takribani miaka miwili mfululizo kutokana na
sababu mbalimbali zilizokuwa zikielezwa na uongozi wa juu.
Hatahivyo, kutofanyika kwa michezo hiyo kumewanyima haki
watumishi wa umma kushindwa kujenga afya zao na kudumisha umoja na urafiki
ikiwa ni pamoja na kukutana na watumishi wengine mbalimbali wa Idara na Wizara
nyingine wakati wa michezo hiyo.
Mbali na kutofanyika kwa michezo hiyo pia kumekuwa hakuna
mabonanza ya kushirikisha idara za serikali na wizara kwa muda mrefu, ambapo
tayari Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika kwa mazoezi
ya viungo angalau mara moja kila mwezi ili kujenga afya kwa watumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment