HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 31, 2018

KAMATI YA MAADILI YA TFF YAMFUNGIA MWENYEKITI WA ABAJALO

Kamati ya Maadili ya TFF iliyokutana Januari 28, 2018 imepitia shauri la mwenyekiti wa Abajalo FC Edgar Chibula lililofikishwa kwenye kamati hiyo na Sektretarieti ya TFF.
HUKUMU
Shauri la Ndugu Edgar Chibula Mwenyekiti wa Klabu ya Abajalo FC lililosikilizwa mbele ya Kamati alishtakiwa kwa kosa la kuongea maneno ya kuikashifu,kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari ikiwa ni kinyume na kifungu cha 50(1), (2) na (6) cha katiba ya TFF toleo la 2015,Vilevile ni kinyume na kanuni ya 15 na 16 ya kanuni za maadili ya TFF toleo la 2013.
MAELEZO YA KOSA
Chibula akiwa Mwenyekiti wa klabu ya Abajalo FC na mjumbe wa Bodi ya Ligi aliongea maneno ya kuikashifu, kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari,Akiwa mmoja wa viongozi wa juu wa mchezo wa mpira hapa nchini hakupaswa kuongea maneno ya kukashfu taasisi anayoiongoza, kwa kufanya hivyo amevunja kanuni ya uwajibikaji wa pamoja na utunzaji wa siri za taasisi.
Kwenye shauri hilo, mtuhumiwa hakuweza kuhudhuria na badala yake alileta utetezi wake kwa njia ya maandishi ambao unakubalika kikanuni. Sekretarieti ya TFF iliwasilisha ushahidi wa sauti (audio clip) ya mahojiano aliyofanya na kituo kimoja cha redio ambapo kwenye mahojiano hayo mtuhumiwa alisikika akitamka maneno hayo yasiyo na afya kwa maendeleo ya mpira wetu.
Pia Sekretarieti ya TFF imewasilisha barua ya utetezi kutoka kwa mtuhumiwa ambapo alikiri kuongea na vyombo vya habari baada ya kufanya kila njia ya kuwasiliana na uongozi wa TFF bila mafanikio. Hata hivyo Kamati haikupata nakala ya mawasialiano hayo kutoka kwa mtuhumiwa. Aidha katika barua hiyo mtuhumiwa aliandika maneno yenye kukera na ya kichonganishi.
Baada ya Kamati kupitia shauri hili imeridhika pasipo na shaka tuhuma dhidi ya mtuhumiwa, kitendo cha kumhusisha mdhamini kwa kuishutumu taasisi inayoongoza mpira ni uchonganishi na ni hatari kwa maendeleo ya mpira; kinaweza kuwaogopesha wadhamini wengine ambao wana nia ya kuwekeza katika mpira,Mtuhumiwa hakuwa na ushahidi wowote uliombatana na tuhuma hizo zinazoweza kudidimiza jitihada za kuinua mchezo wa mpira nchini.
Kamati imemtia hatiani Bw. Edgar Chibula kwa kosa la kuongea maneno ya kuikashifu, kuidhalilisha na kuivunjia heshima TFF katika vyombo vya habari ikiwa ni kinyume na kifungu cha 50 (1), (2) na (6) cha katiba ya TFF toleo la 2015. Hivyo Kamati inamuhukumu kifungo cha kutojihusisha na shughuli za mpira kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) na faini ya shilingi milioni tatu (sh.3,000,000) chini ya kifungu cha 73(4) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.
TFF YASIKITISHWA NA UPOTOSHAJI ULIOFANYWA NA GOLIKIPA WA SHUPAVU FC
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF limesikitishwa na kauli iliyotolewa na golikipa wa timu ya Shupavu ya Morogoro Halifa Mgwira baada ya kumalizika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho la Azam ASFC dhidi ya Azam FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro. 
 
Wakati akifanyiwa mahojiano Mgwira alizungumza maneno yanayoashiria kuwa wamefungwa kwasababu TFF haijawapa pesa ambazo wanazitumia kwaajili ya chakula. 
 
Utaratibu wa TFF ni kuzipatia pesa timu kabla ya kucheza mechi zao utaratibu ambao umefanyika kwa Shupavu waliolipwa pesa zao jana ikiwemo na TFF kuwaongeza fedha ya ziada mara mbili zaidi kama yalivyokuwa maombi yao. 
 
TFF inafanya utaratibu wa kumtaka Mgwira kuthibitisha madai yake na endapo atashindwa kuthibitisha ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni.
 
TFF inasisitiza kwa wanafamilia wa mpira wa miguu kufuata taratibu katika kuwasilisha malalamiko yao kwakuwa taratibu ziko wazi.
 
VIONGOZI WA TFF WAENDA KWENYE MKUTANO MKUU CAF
Viongozi watatu wa juu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF watahudhuria mkutano mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa CAF utakaofanyika Februari 2, 2018 nchini Morocco.
Mbali na Rais wa TFF Ndugu Wallace Karia wengine watakaohudhuria mkutano huo ni Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred.
 IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF

No comments:

Post a Comment

Pages