Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 31 Januari, 2018 amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Tumaini Jijini Dar es Salaam akiwemo muigizaji mkongwe nchini Mzee Amri Athuman, maarufu kwa jina la “King Majuto”.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi namba 3 hadi namba 8 na baadaye akamuona King Majuto ambaye anaendelea kupata matibabu ya tezi dume.
King Majuto amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kwenda hospitali kumuona na amempongeza kwa namna anavyosimamia huduma za afya nchini, kwani tangu maradhi yalipomuanza amehudumiwa vizuri na ana matumaini ya kupona na kurejea katika majukumu yake ya kila siku.
Aidha, King Majuto amemuombea Mhe. Rais Magufuli ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuongoza nchi vizuri, na amebainisha kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano zimerejesha nidhamu, zimeongeza uchapakazi, zimesaidia kukabiliana na wizi na zimeongeza heshima ya nchi.
“Kiongozi lazima awe namna hii, sio kuleta mzahamzaha, ukisema jambo watu wanatekeleza, wezi wanakamatwa, wala rushwa wanakamatwa, wenye vyeti feki hata kama amefanya kazi miaka 20 fukuza, hii safi, sasa kuna heshima na watu wanachapa kazi, ndio maana mimi hata wakati wa kampeni niliwaambia wasanii wenzangu hapa Rais ni Magufuli” amesema King Majuto.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
31 Januari, 2018
No comments:
Post a Comment