WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
hajaridhishwa na ubora wa ujenzi wa kituo cha forodha cha Sirari kilichopo
kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.
Kufuatia hali hiyo amemtaka Kamishna
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
afike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma akiwa na mkandarasi aliyejenga
kituo hicho.
“Serikali haiwezi kuvumilia ujenzi
wa hovyo kiasi hiki, namtaka Kamishna wa TRA aje ofisini kwangu Januari 25,
2018 pamoja na mkandarasi aliyejenga kituo hiki akiwa na nyaraka zote za ujenzi
wa jengo hilo.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano,
Januari 17, 2018) mara baada ya kumaliza kukagua kituo hicho kilichopo wilayani
Tarime, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Waziri Mkuu amesema hajaridhishwa na
ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka
2011 na kukamilika mwaka 2014.
Waziri Mkuu amejionea mwenyewe kuta
za jengo hilo zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi
za baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amewataka wananchi wa wilaya hiyo kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kuzingatia
sheria na wajiepusha na biashara za magendo.
Waziri Mkuu amesema magendo
yanaikosesha Serikali mapato, hivyo bidhaa yoyote itakayokamatwa ikiingizwa
nchini kwa njia za magendo itataifishwa pamoja na chombo cha usafiri
kilichotumika.
Pia Waziri Mkuu ametembelea shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Borega, ambapo amewasisiza wananchi wasimamie elimu
ya watoto wa kike ili wafikie malengo yao.
Amesema Serikali imeweka sheria kali
kwa yeyote atakayekatisha masomo kwa watoto wa kike iwe kwa kumpa ujauzito au
kumoa, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka
wanafunzi hao wasome kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kamwe
wasijihusishe katika mambo ambayo hayahusiani na masomo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, JANUARI 17, 2017.
No comments:
Post a Comment