Mhandisi Astelius John kutoka Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania akitoka kuweka alama ya kuondolewa kwa moja ya
nyumba zilizolipwa fidia eneo la Kipunguni A
Moja ya
Nyumba zilizoanza kubomolewa na mwananchi mwenyewe katika eneo la
Kipunguni A.
Afisa ardhi Mkuu kutoka Mamlaka ya viwanja Vya
Ndege Bi Cecilia Mwing’uri
akisaidia zoezi la kuweka alama
ya kuondoa nyumba hiyo kati ya nyumba
59 zinazotakiwa kubomolewa.
Na Mwandishi Wetu, TAA
JOPO la maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), limefanya
utambuzi wa nyumba 59 zilizopo eneo la Kipunguni A, jijini Dar es Salaam
na kutoa notisi ya siku saba kwa wakazi wake kuhama.
Nyumba hizo ni zile ambazo serikali tayari ililipa wakazi wake stahiki
zao mwaka 2014 kufuatia uthamini uliofanyika mwaka 1997, lakini bado wanachi
hao waliendelea kuishi eneo hilo linalohitajika na Serikali kwa ajili ya
matumizi ya shughuli za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo ya utambuzi
iliyofanyika leo Januari 25, Ofisa Ardhi mkuu wa TAA, Cecilia Mwing'uri
amesema jopo hilo lilijumuisha watumishi kutoka TANESCO, Polisi, TAA kitengo cha sharia na Mahusiano, na wajumbe wa eneo hilo waliowawakilisha
wananchi.
"Tulizitambua nyumba husika na kuziwekea alama ya X na kutoa notisi
ili wakazi ambao bado wapo eneo hilo la Kipunguni wahame ndani ya siku
saba kuanzia leo.
"Kwa bahati nzuri kuna ambao wamehama na wengine wanaendelea na
ubomoaji wa kistaarabu wa nyumba zao isipokuwa wachache ambao waliuziwa
nyumba na maeneo huku wamiliki
wa kwanza wakijua fika, eneo hilo ni mali ya serikali na walishalipwa
fedha zao," amesema.
Kwenye zoezi hilo Bi Cecilia
alisema watumishi wa Shirika la Umeme (TANESCO), kutoka mkoa wa kihuduma
wa Gongo la Mboto walitoa siku tatu kuanzia kesho na kwamba baada ya hapo
wataanza zoezi la kuondoa miundombinu ya umeme kwenye nyumba husika
ili kurahisisha zoezi la ubomoaji.
Mwishoni mwa mwaka jana, wakati wa ziara ya Naibu waziri wa mawasiliano
na uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye kwenye makao makuu ya TAA,
alikutana na hoja hiyo na kuagiza Mamlaka hiyo ya Viwanja vya Ndege
kuhakikisha waliolipwa fidia na bado wapo Kipunguni A wanaondoka ndani ya
siku 30.
Amesema kwa kuwa serikali tayari imekamilisha jukumu lake kwa nafasi
yake, hakuna budi watu hao wakahama ili nia ya serikali kwenye eneo hilo
kama ni upanuzi wa kiwanja cha ndege au shughuli nyingine itekelezwe kwa
nafasi.
Katika mazungumzo yake na watumishi wa TAA akiwemo Mkurugenzi Mkuu,
Richard Mayongela, Mhandisi Nditiye aliahidiwa kuwa mamlaka hiyo
itahakikisha wakazi ambao tayari wamelipwa fidia katika awamu iliyohusisha
nyumba 59 inatekelezwa, kama ambavyo TAA imeanza kufanya leo.
No comments:
Post a Comment