*Asisitiza
kahawa iuzwe kwa mfumo wa ushirika
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wajikite
kwenye zao la kahawa ili wawe na zao mbadala la biashara.
Ametoa wito huo
leo (Ijumaa, Januari 5, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha
Lipokela na vijiji jirani, wilayani Songea mara baada ya kukagua shamba la
kahawa la Aviv Tanzania lenye ukubwa wa hekta 1,990.
“Limeni kahawa
ili mpate fedha sababu zao hili ni la biashara. Kahawa ni miongoni mwa mazao
matano ya biashara ambayo Serikali ya awamu ya tano imeamua kuyawekea mkazo ili
yaweze kuongeza tija kwa wakulima na kuinua uchumi wa Taifa”.
“Tumeamua kuweka
mkazo kwenye mazao matano ya pamba, kahawa, chai, korosho na tumbaku kwa sababu
yanaleta tija na kuliingizia Taifa fedha za kigeni,” alisema na kuongeza:
“Tumefanya
tathmini na tumegundua udhaifu mkubwa mkubwa katika usimamizi wa mazao haya
ndani ya Serikali kuanzia ngazi ya Halmashauri.”
Waziri Mkuu
alisema ni lazima wananchi walime zao hilo na viongozi wahakikishe wananchi
wananufaika za zao hilo. Hata hivyo, alionyeshwa kutoridhishwa na utendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Songea baada ya kuelezwa kuwa kampuni ya Aviv Tanzania
imezalisha miche milioni moja lakini iliyochukuliwa na kusambazwa kwa wananchi
ni miche isiyozidi 200,000.
“Kampuni hii
imeamua kutoa miche ya bure kwa wakulima, wamezalisha miche milioni moja lakini
hadi sasa imechukuliwa 200,000 tu. Kuna miche zaidi ya 800,000, imebaki, na
tena wawekezaji hawa wanatoa elimu bure ya kulima na kuitunza mikahawa yako,”
alisema.
Amewataka
wakulima hao watenge ekari moja hadi tatu kwa kila kaya ili waweze kulima zao
hilo. “Wana Lipokela tengeni ekari moja hadi tatu za kulima kahawa, tukifanya
hivyo suala la fedha kupitia kahawa litakuwa limekamilika,” alisema.
Amesema itabidi
zao la kahawa liundiwe mfumo maalum wa ununuzi ambao ni wa ushirika kwa
kuzingatia vyama vya msingi (AMCOS) vilivyokuwepo.
Mapema, akitoa taarifa juu ya shamba hilo, Meneja wa Aviv
Tanzania, Bw. Medu Medappa alisema lengo la kuanzisha mradi huo lilikuwa ni
kuhakikisha wanapata shamba kubwa la kahawa aina ya Arabica nchini Tanzania
lenye viwango vya kimataifa.
Alisema wamekwishatoa
ajira kwa Watanzania wapatao 3,000 zikiwemo za moja kwa moja na za msimu.
Alisema kampuni
hiyo imeweza kuchangia miradi ya maendeleo kwenye vijiji vinne jirani vya Lipokela,
Lusonga, Liganga na Selekano. “Hadi mwaka 2017 tuliweza kukamilisha ujenzi wa
zahanatio katika kijiji cha Lipokela, nyumba ya mwalimu katika vijiji vya
Liganga na Lusonga, uchangiaji wa madawati kwenye vijiji vya Lipokela na Lusonga,”
alisema.
Alisema
wameweza kuanzisha scheme ya wakulima wadogo wa nje (outgrowers scheme) kwa
wakulima 2,000 ambao wamegawanyika kwenye vikundi 36 katika vijiji 31 ndani ya
mkoa wa Ruvuma.
Waziri Mkuu
anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea wilaya ya
Mbinga ambako atakagua miche kwenye taasisi ya TACRI, atatembelea kiwamda cha
kukoboa kahawa cha Mbinga (MCCCO), kuzungumza na watumishi na madiwani na pia
kuhutubia mkutano wa hadhara.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA,
JANUARI 5, 2018.
No comments:
Post a Comment