WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati ya kutosha
itakayowezesha pamba yote inayolimwa nchini kununuliwa na tayari
imeshaanza mchakato wa kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Februari 8, 2018) Bungeni
mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Sumve, Bw. Richard
Ndassa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Bw.
Ndassa alitaka kujua Serikali imejipangaje kuwasaidia wananchi
walioitikia wito wa kulima pamba iwapo wanunuzi watashindwa kununua
pamba yote.
Mbunge
huyo ameongeza kuwa mwaka jana, Waziri Mkuu aliwaita viongozi wa mikoa
inayolima pamba na kuwapa maelekezo ya kwenda kufufua zao hilo ambapo
wakulima waliitikia wito na mwaka huu wanatarajia kupata mavuno mengi.
Waziri
Mkuu amesema ni kweli kuwa mwishoni mwa mwaka jana, Serikali iliwaita
viongozi hao ambao ni Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya
ambao walipewa maelekezo ya kwenda kuhamasisha kilimo cha zao hilo na
kuwasaidia wakulima kuanzia ngazi ya awali.
Waziri
Mkuu amesema Serikali inashiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la
pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba kwa kulima kitaalam,
upatikanaji wa pembejeo hadi masoko.
“Mimi
mwenyewe mwezi huu nitakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mwanza, kwa hiyo
kati ya tarehe 15-17, nimeitisha mkutano wa wafanyabiashara wote wa
pamba nchini iwe ni wanaosokota nyuzi, kuchambua pamba au kukamua pamba,
ili mradi wanajihusisha na pamba,” amesema.
Ili kupata uhakika wa masoko nje ya nchi, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Kampuni
ya Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) inawasiliana na mataifa mbalimbali ili
kuhakikisha pamba yote iliyolimwa nchini inanunuliwa.
“Serikali
imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji
wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba. Mengine ni korosho,
kahawa, chai na tumbaku, yote kwa pamoja yanachangia kukuza uchumi,”
amesema.
Amesema
awali wakulima wa mazao makuu matano ya biashara nchini likiwemo na zao
la pamba walipunguza uzalishaji baada ya kukosa usimamizi hali
iliyoilazimu Serikali ichukue uamuzi wa kuyafufua kwa kuwa historia
inaonyesha kwamba mazao hayo yanachangia katika ukuaji wa uchumi wa
Taifa.
Akijibu swali kuhusu
ukosefu wa dawa za kuulia wadudu ambalo Bw. Ndassa alilalamikia, Waziri
Mkuu amesema Serikali imeendelea kuagiza dawa hizo kwa kuwa ni sehemu
ya mahitaji ya kilimo cha zao la pamba.
“Wiki
iliyopita niliona kwenye habari Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba akipokea
chupa zaidi za milioni moja na akasema kuwa kuna dawa nyingine chupa
zaidi ya milioni mbili zinakuja.”
“Ni
jukumu la Bodi hiyo kuhakikisha kuwa dawa za zao la pamba, ziwe za maji
au za kupulizia zinapatikana nchini na zinapelekwa kwa wakulima,”
alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, FEBRUARI 8, 2018.
No comments:
Post a Comment