WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka viongozi wa mkoa wa Mtwara kupambana na makundi ya watu yanayotaka
kuharibu masoko ya korosho.
Hatua hiyo imekuja baada ya
kuwepo kwa mnunuzi aliyekataa kununua korosho kutokana na kutoridhishwa na
kiwango cha ubora wa korosho alichokikuta ghalani.
Ametoa agizo hilo leo
(Jumatano, Februari 28, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa
Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba.
“Tandahimba korosho zote ni
daraja la kwanza sasa korosho chafu zinatoka wapi? Kuna kundi linataka kuharibu
soko lazima tupambane nalo.”
Waziri Mkuu ameongeza
kuwa “lazima mshirikiane kuwabaini
walioleta korosho chafu Tandahimba na wakipatikana wachukuliwe hatua kali za
kisheria.”
Amesema haiwezekani mnunuzi
amenunua korosho daraja la kwanza alafu anakuja anakuta korosho nyingine tena
chafu, lazima waliozibadilisha wasakwe.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha
kubangua korosho cha Amama Farms, ambapo ametoa wito kwa walionunua viwanda vya
korosho wafunge mashine mpya na kuanza uzalishaji.
Hata hivyo amewataka wamiliki
wa viwanda vyote vya kubangulia korosho washirikiane na Serikali katika kufuata
utaratibu wa kununua korosho.
Pia Waziri Mkuu amezindua
barabara yenye urefu kilomita tatu iliyojengwa kwa kiwango cha lami ambayo
imegharimu sh. bilioni 1.38 zilizotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya
wilaya ya Tandahimba.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda hicho Kwa
Mahmoud Sinani alisema korosho zinazobanguliwa kiwandani hapo zinauzwa ndani na
nje ya nchi.
Amesema katika awamu ya
kwanza ya uwekezaji huo umegharimu sh. bilioni 12 na wanatarajia kuendelea na
awamu ya pili ambapo watawekeza dola milioni 20.
Amesema kwa sasa kiwanda
hicho kimeajiri watumishi 250 na wanatarajia kuajiri watumishi 1,500 mara baada
ya kumaliza awamu ya pili ya upanuzi wa kiwanda.
Pia Waziri Mkuu amewapongeza
watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba kwa kuweka kipaumbele katika
ujenzi wa miundombini ya barabara kwa kiwango cha lami.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 28,
2018.
No comments:
Post a Comment