*Asisitiza ulemavu si
kigezo cha kukosa elimu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wazazi na walezi wa watoto wenye mahitaji maalumu kutowafungia ndani
na badala yake wawapeleke shule.
Amesema ulemavu si kigezo cha
kuwakosesha watoto hao kupata elimu na kufanya kazi, hivyo amewataka jamii
kutowakatisha tamaa
Alitoa agizo hilo jana
(Jumanne, Februari 27, 2018) wakati alipokagua mradi wa ujenzi wa majengo ya
chuo cha Ualimu Kitangali, kilichopo Newala mkoani Mtwara.
“Watakaobainika kuwafungia
ndani watoto wenye mahitaji maalumu wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu wanawakosesha
haki ya kupata elimu.”
Pia amewaagiza watendaji wa
vijiji wafanye sensa katika maeneo yao ili kubaini idadi ya watoto hao na
watakapofikia umri wa kwenda shule wapelekwe.
Waziri Mkuu alisema Serikali
inataka watoto wenye mahitaji maalumu watambulike pamoja na mahitaji yao na
waliofikia umri wa kwenda shule wapelekwe.
“Tunataka kila mtoto wa
Kitanzania aliyefikia umri wa kwenda shule apelekwe shule na kusoma na wenzake.
Serikali imeboresha elimu ili watoto wote wasome”.
Alisema watoto wenye mahitaji
maalumu wana haki sawa na wengine, hivyo hakuna sababu ya kuwafungia ndani na
kuwakosesha kupata elimu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo alisema mradi huo
unahusisha ujenzi na ukarabati wa vyuo vinne vya ualimu.
Dkt. Akwilapo alivitaja vyuo
hivyo ni Ndala cha Tabora, Mpuguso cha Mbeya, Kitangali cha Newala na
Shinyanga, ambapo ujenzi utagharimu sh. bilioni 36.47.
Alisema mradi huo wa ujenzi
na ukarabati wa miundombinu katika vyuo hivyo vinne utaleta tija kubwa kwa
Serikali katika kuongeza fursa za kutoa mafunzo ya ualimu katika ngazi za
stashahada na shahada.
“Vyuo vyote hivi vinne
vitakapokamilika vitakuwa na uwezo wa kudahili wanachuo 3,300 kwa wakati mmoja
kutoka uwezo wa sasa wa kudahili wanachuo 1,855”.
Akizungumzia kuhusu chuo cha Kitangali
ambacho kilijengwa 1937, alisema kinajengwa upya kutokana na uchakavu wake
kiasi cha kutofaa kufanyiwa ukarabati.
Awali, Kaimu Mkuu wa chuo hicho Mwalimu
Emmanuel Haule alisema Serikali kwa kushirikiana na Canada zimetoa sh. bilioni
8.26 za ujenzi wa miundombinu.
Mwalimu Haule alisema
miundombinu inayojengwa chuoni hapo ni pamoja na vyumba vya madarasa, mabweni,
nyumba za watumishi na maabara.
“Pia tunajenga ukumbi wa
mikutano na ukumbi wa mihadhara, maktaba na uchimbaji wa kisima cha maji.
Ujenzi unatarajiwa kukamilika Aprili 26, 2018.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 28,
2018.
No comments:
Post a Comment