NA SULEIMAN MSUYA
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimekutana na
Mkurugenzi Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya International
Republican (IRI) Peter Okong'o na kuzungumza juu ya hali ya kisiasa nchini
Tanzania na umuhimu wa wadau wote kushirikiana kuhakikisha demokrasia ya
Tanzania inalindwa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro katika taarifa yake aliyotoa kwa vyombo
vya habari jana baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
“Nimemweleza ndugu Okong'o kuwa, wao IRI
wanaweza kuendelea na kazi ya kushauri vyama vya siasa, serikali, taasisi za
kidemokrasia, lakini kwa kweli sisi viongozi wa vyama na watanzania ndiyo wenye
jukumu la kupigania haki na mabadiliko ya kweli,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema baada ya maelezo ya
kutosha kutoka CUF, Okong'o amewahakikishia kuwa taasisi yao itaendelea na
juhudi zake za kufanya kazi na serikali wadau wote ili kujenga uwezekano wa
kujenga utangamano na mabadiliko yanayotakiwa na wananchi.
“Nimemhakikishia kuwa CUF na viongozi wake
wako imara na watatoa mchango wao kwa nchi yao bila kukata tamaa, maana
mabadiliko hayataletwa kwenye sahani bila kupiganiwa na wadau,” alisema.
Mtatiro alisema Okong'o yumo katika ziara
maalim ya kuwatembelea wakuu wa vyama hapa nchini Tanzania, taasisi za kiraia,
taasisi za usimamizi wa uchaguzi (NEC na ZEC) na Serikali.
Alisema IRI ni taasisi isiyo ya Kiserikali na
kisiasa lakini imejikita katika kushauri kuhusu uhuru na demokrasia duniani
ikiwemo na kusaidia vyama vya siasa ili viweze kufikisha ujumbe kwa wananchi
kuhusu mipango mbalimbali ambayo Serikali imeweka kuhusu wao.
No comments:
Post a Comment