NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
MSIMU wa 11 wa mbio za Ngorongoro ‘Ngorongoro Race’ unatarajiwa kufanyika mjini Karatu mkoani Arusha, Aprili 21 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini hapa, Mratibu wa Ngorongoro Race, Meta Petro, alisema mbio hizo zilianza mwaka 2008, zikiwa na lengo la kutumia michezo kupaza sauti ili kukuza vipaji vya wachezaji wa riadha na kumaliza matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii, kwa kuzingatia maeneo ya Karatu na Ngorongoro mkoani Arusha.
Petro, alifafanua kuwa, Ngorongoro Race huwa na vipengele vitatu, Mbio za Kilomita 21 ‘Half Marathon’, ambazo huanzia Lango la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuishia viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu, Mbio za Kilomita 5 ‘Fun Run’ ambazo pia huhusisha washiriki binafsi, Taasisi na Kampuni mbalimbali huku Kilomita 2.5 zikiwa maalumu kwa watoto hususan wa shule za msingi.
“Mashindano haya yamekuwa chachu kwa kusaidia wachezaji kama daraja la kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa, kwani Klabu zote za michezo za ndani ya nchi na baadhi ya klabu za nje pia hualikwa kushiriki,” alisema Petro na kuongeza.
Kama tulivyoainisha awali, kuwa lengo kubwa ni kukuza vipaji vya wachezaji na kusaidia matatizo ya kijamii, tokea kuanzishwa kwake Ngorongoro Race imeweza kusaidia tatizo la malaria kwa miaka zaidi ya saba na kuwezesha upungufu wa maambukizi kutoka asilimia 8.0 mwaka 2008 hadi kufikia asilimia 0.4 kwa mwaka 2014 kwa Wilaya ya Karatu kwa mujibu wa takwimu za Mganga Mkuu wa Mkoa na Wizara ya Afya.
Aidha, alisema pia zilisaidia ujenzi wa shule ya awali kwa watoto wa jamii ya Kimasai huko Endulen wilayani Ngorongoro, ambapo wanafunzi hawakuwa na shule, kitu ambacho kilididimiza ndoto zao za kuwa nguvu kazi ya taifa.
“Kwa upande wa michezo, tokea kuanzishwa kwake Ngorongoro Race, wachezaji mbalimbali wameweza kupanda ngazi toka mashindano ya Klabu hadi ngazi za Kitaifa na kimataifa kama Alphonce Felix Simbu, Fabian Joseph, Failuna Abdi, Jackline Sakilu na wengineo wengi,” alisema.
Mratibu huyo, alibainisha kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka jana, mashindano hayo yamekuwa yakibeba ujumbe wa kupiga vita ujangili dhidi ya wanyama pori, hasa kwa kuzingatia kuwa biashara hiyo haramu kwa sasa imekuwa tishio kwa rasilimali za Taifa wakiwemo Tembo, Faru na wanyama wengineo.
“Kwa muda wote huo tunapenda kuwashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakituunga mkono, wakiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bonite Bottlers, Zara Tours, Kampuni ya mawasiliano ya Tigo, Patamu Restaurant, Roy Safari, New Sparrow Lounge, Red Bulls, Aceme Events Managements na wengineo,” alisema na kutoa wito kwa kampuni na wadau mbalimbali, nafasi iko wazi kujiunga mwaka huu katika kuhakikisha tukio hillo linazidi kufana.
No comments:
Post a Comment