HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 07, 2018

Utaratibu mpya wanariadha kwenda nje

NA MWANDISHI WETU


SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limesema kuanzia hivi sasa utaratibu wa wanariadha wanaotaka kwenda kushiriki mashindano mbalimbali nje ya nchi umebadilika ambako mbali na kupata baraka za shirikisho lazima Baraza la Michezo la Taifa (BMT), libariki.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday (Pichani), wamepokea maagizo kutoka serikalini juu ya mabadiliko hayo.

“Kuanzia sasa wanariadha watakaoalikwa kushiriki mashindano mbalimbali nje ya nchi ni lazima wapate vibali BMT, Shirikisho la Riadha litaendelea kutoa barua ya kuambatana na mwaliko, halafu barua hizo mbili (mwaliko na barua ya RT), vyote vipelekwe BMT siku 14 kabla ya siku ya safari yenyewe,” alifafanua Gidabuday na kuongeza.

Hivyo nachukua nafasi hii kuwataarifu wahusika wote kwamba, nitasimamia maagizo ya serikali ipasavyo… Nawaagiza makocha na mameneja wa ndani, wafanye juhudi zao wenyewe kuwataarifu waandaaji wa mbio za kimataifa, kuleta mialiko mapema ili RT tuweze kushughulikia kiutendaji ndipo ziende BMT.

Gidabuday, aliwasisitiza wahusika wafuate utaratibu mpya, vinginevyo safari nyingi zitakuwa zinakwama kwani RT haitashughulikia mwaliko ambao utachelewa.

“Ndiyo maana pamoja na kuwaandikia barua wahusika, nimeamua kutumia vyombo vya habari ili ujumbe huu muhimu umfikie kila anayehusika ili kuepusha athari zinazoweza kutokea kwa kutofuata taratibu hizi mpya,” alisema Gidabuday.

No comments:

Post a Comment

Pages