HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 18, 2018

WAZIRI NCHEMBA KUBEBA TAMASHA LA PASAKA 2018

.Uhondo wapelekwa Kirumba, Simiyu

NA MWANDISHI WETU

JOTO la tamasha la Pasaka litakalotikisa Kanda ya Ziwa katika mikoa ya Mwanza na Simiyu kuanzia Aprili mosi na pili, limezidi kupanda baada ya waratibu wa tukio hilo kumtaja Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuwa mgeni rasmi.
Alex Msama


Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama, Waziri Nchemba ndiye atawaongoza maelfu katika tukio hilo la kusindikiza tukio la ushindi wa wanadamu dhidi ya dhambi kupitia ufufuko wa Yesu Kristo.

Msama alisema Waziri Nchemba atakuwa mgeni rasmi akimwakilisha Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu ambaye licha ya kukubali kubeba tukio hilo, siku hiyo atakuwa na majukumu mengine.

Alisema kutokana na Waziri Nchemba kukubali kubeba heshima ya tukio hilo, Kamati yake imejipoanga kuhakikisha kila atatakayefika katika Uwanja wa Kirumba Aprili mosi na kule Simiyu, hatajutia muda na kiingilio chake.
Mwigulu Nchemba


“Tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa kila atakayeingia uwanjani hatajutia muda na fedha yake kwa kupata alichokitaraji ambacho ni baraka kutoka kwa waimbaji mahiri ambao kwa sasa wapo kambini wakijifua kufanya kweli,” alisema Msama.

Kwa upande wa waimbaji, Msama alisema hadi sasa tayari waimbaji wengi wamekaa mkao wa utayari wakiongozwa na malkia wa Muziki wa injili nchini, Rose Muhando ambaye atatumia tamasha hili kuzindua albamu yake mpya ya ‘Usivunjike Moyo.’

Waimbaji wengine katika tukio hilo la kuutukuza ufalme wa Mungu, ni Angel Benard, Paul Clement, Christina Shusho, Beatrice Mwaipaja, Bonny Mwaitege, Ephraem Sekereti kutoka Zambia, Jesca Honole na wakali wengine.

Viingilio vya tukio hilo ni kwamba, katika Uwanja wa CCM Kirumba; wakubwa watalipa sh 5,000 huku watoto wakilipa 2,000 na mkoani Simiyu; wakubwa watalipa sh. 3,000 na watoto itakuwa shilingi 2,000.

Msama ametoa wito kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili kwa mikoa uya Kanda ya Ziwa, kujitokeza kwa wingi kuunga mkono uamuzi wa Msama Promotions kutoa upendeleo maalumu wa Tamasha hilo kufanyika Mwanza na Simiyu pekee.

“Nawaomba wapendwa katika Kristo Yesu na wadau wa muziki wa injili kwa ujumla, wajitokeze kwa wingi katika uwanja wa CCM Kirumba na kule mkoani Simiyu, kupata baraka za neno la Mungu kupitia nyimbo za waimbaji mahiri walioandaliwa,” alisema.

Tamasha hilo lenye umri wa miaka 18 sasa tangu kuanzishwa kwake, limekuwa na malengo mengi ndani yake ikiwemo kueneza ujumbe wa neno la Mungu na sehemu ya mapato kufariji makundi maalumu kama walemavu, yatima pamoja na wajane.

No comments:

Post a Comment

Pages