HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 03, 2018

Mtanzania awekewa pingamizi Madola

TIMU ya Taifa ya Tanzania ya Jumuiya ya Madola, imetikiswa baada ya Afrika Kusini kumwekea pingamizi mmoja wa wachezaji wake.

Mchezaji aliyewekewa pingamizi ni Mwanariadha Anthony Mwanga, ambako Afrika Kusini inapinga kuichezea Tanzania ikidai ni mali yao.

Mwanga anayeshiriki Kuruka chini, anasoma nchini Afrika Kusini.

Shirikisho la Riadha la Afrika (ASA), juzi lilipeleka pingamizi hilo Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), likiwasilisha vyeti vya kuzaliwa vya Mwanga ambaye alizaliwa Afrika Kusini wazazi wake walikokuwa wakifanya kazi.

Baada ya IAAF kupata madai hayo ya ASA ililitaka Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kujibu hoja hiyo.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday, walipata ‘e mail’ kutoka Monaco Ufaransa makao makuu ya IAAF, wakitaka uthibitisho wa uraia wa mchezaji huyo haraka walifanya hivyo kwa kutuma nakala ya pasi yake ya kusafiria.

“Unajua Afrika Kusini ndio wawasilisha pingamizi IAAF wakitaka Mwanga asishiriki michezo hiyo, huku wakiwasilisha nakala ya vyeti vya kuzaliwa ambavyo kweli vinaonyesha alizaliwa huko…Lakini ukweli huyu kijana ni Mtanzania ila wazazi wake walikuwa wakifanya kazi huko,” alisema Gidabuday na kuongeza.

Ila tuliwajibu Monaco haraka na wakatuelewa, kabla ya kututaka tena tuwasilishe uthibitisha wa uraia wa mzazi wake, hivyo tukatuma tena nakala ya pasi ya kusafiria ya Mzazi wake Dk. Tapson Ally Mwanga ambaye ni mzaliwa wa Hai Kilimanjaro na hapo tukawa tumesawazisha kila kitu.

Gidabuday, alieleza kushangazwa na hatua hiyo ya Afrika Kusini, ambayo alidai inalenga kumtoa mchezoni kijana huyo, ila wanashukuru wamevuka kiunzi hicho.

Katibu huyo, alisema licha ya kijana huyo kuchanganywa kidogo na jambo hilo, ila hivi sasa katulia na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Tanzania katika michezo hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Aprili 5 hadi 15 huko Gold Coast Australia, inawakilishwa na michezo ya Riadha, Kuogelea, Mpira wa Meza na Ngumi.

No comments:

Post a Comment

Pages