WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha vyama
vya msingi vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha mazao ya
kimkakati ya biashara ya pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku.
Amesema katika mwaka 2018/2019, Serikali inalenga kuimarisha masoko ya
mazao hayo kwa kuhamasisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo mazao hayo
yatazalishwa na kuuzwa kupitia vyama vya ushirika kwa njia ya minada.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati
akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka
2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019 kwenye mkutano wa
11 wa Bunge.
Waziri Mkuu amesema pamoja na hatua hizo, Soko la Bidhaa ambalo
limeshaanzishwa, litasaidia sana kuimarisha masoko ya mazao kwani yatakuwa
yanauzwa kwa njia ya ushindani mkubwa huku wakulima wanaozalisha kwa ubora
wakinufaika na bei ya juu zaidi.
“Serikali imeamua kuweka
mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao matano ya biashara ambayo ni chai,
kahawa, korosho, pamba na tumbaku. Lengo ni kuongeza mapato ya wakulima, kuwa
chanzo cha kuaminika cha malighafi katika uchumi wa viwanda, na kuendelea kuwa
chanzo kikuu cha ajira na fedha za kigeni.
Amesema uamuzi wa kuongeza
usimamizi katika uzalishaji wa mazao hayo makuu ya biashara unatokana na ukweli
kwamba, kwa kipindi kirefu uzalishaji ulishuka kutokana na changamoto kadhaa.
“Miongoni mwa changamoto
hizo ni kupungua tija katika uzalishaji, baadhi ya wakulima kuacha kulima mazao
hayo kutokana na kukata tamaa kwa sababu mbalimbali zikiwemo vyama vya ushirika
kutotekeleza vema wajibu wao, wizi, dhuluma na pia ushiriki mdogo wa maafisa
kilimo katika kusimamia kilimo cha kitaalamu,” alisema.
Alizitaja sababu nyingine za
kushuka uzalishaji wa mazao hayo kuwa ni huduma zisizoridhisha za ugani na
utafiti, ukosefu wa pembejeo bora, utitiri wa tozo na wingi wa vyama vya msingi
na vyama vikuu vya ushirika.
Akitolea mfano, Waziri Mkuu
alisema uzalishaji wa pamba ulipungua kutoka tani 456,814 mwaka 2013/2014, hadi
tani 282,809 mwaka 2015/2016. Kwa upande wa tumbaku, Waziri Mkuu alisema
uzalishaji katika kipindi cha miaka minne ulishuka kutoka tani 126,624 mwaka
2010/2011 hadi kufikia tani 60,929 mwaka 2015/2016.
“Serikali imechukua hatua za
kuimarisha utawala bora kwenye vyama vya ushirika kwa kusimamia chaguzi za
vyama 2,537, chaguzi za viongozi wa bodi za vyama vya ushirika 532 na kufanya
kaguzi katika vyama vya ushirika 2,896 vikiwemo vyama vikuu. Kazi za kusimamia
vyama vya ushirika zinaendelea,” alisema.
Wakati
huohuo, Waziri
Mkuu alisema Serikali inasimamia uendelezaji wa mazao hayo moja kwa moja
kupitia maafisa kilimo na Bodi za Mazao na kwamba imechukua hatua za kufuta
baadhi ya tozo zilizokuwa kero katika mazao makuu ya biashara pamoja na
kuhakikisha kwamba mauzo yanafanyika kwa njia ya wazi na inayoleta ushindani.
“Kutokana na hatua
zinazochukuliwa na Serikali kusimamia mazao makuu ya biashara, tayari tumeanza
kuona matokeo chanya kwa kuongezeka uzalishaji wake. Kwa mfano, hadi mwezi Machi
2018, uzalishaji wa mazao ya asili ya biashara ulifikia tani 804,025.
Uzalishaji huu unaashiria ongezeko la mavuno ikilinganishwa na mwaka 2016/2017.
Ongezeko hilo la uzalishaji wa mazao ya biashara linakwenda sambamba na
kuimarika kwa mwenendo wa bei za mazao hayo hususan korosho na kahawa,” alisema.
Waziri Mkuu aliliomba Bunge likubali kupitisha sh.
143,618,762,698 zikiwa ni makadirio
ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizopo
chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2018/2019 ambapo sh. 74,527,321,698
ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 69,091,441,000 ni kwa ajili ya
matumizi ya maendeleo.
Vilevile, Waziri
Mkuu aliliomba Bunge liidhinishe sh. 125,521,100,000 kwa ajili ya Mfuko wa
Bunge ambapo sh. 117,205,487,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh.
8,315,613,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO,
APRILI 4, 2018
No comments:
Post a Comment