*Mapato
yapanda kutoka sh. milioni 147 hadi sh. milioni 714
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa Mererani
kutasaidia kuongeza mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya wizi na utoroshaji wa madini ya Tanzanite.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 10, 2018) Bungeni mjini Dodoma kwenye mkutano
wa 11 wa Bunge, wakati akihitimisha mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa kazi
za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka
2018/2019.
Waziri
Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa ukuta
huo uliozinduliwa Aprili 6, mwaka huu Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kutasaidia
pia kudhibiti ulanguzi na biashara ya magendo pamoja na kuimarisha usalama kwenye mgodi, kwa wafanyakazi na
wafanyabiashara wa Tanzanite.
“Kukamilika kwa ujenzi huo pia kutasaidia kuongeza mapato ambapo katika kipindi cha Januari hadi Machi 2018, Serikali imekusanya takriban shilingi milioni 714 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi
milioni 147.1 kwa mwaka mzima wa 2017,”
alisema.
Waziri Mkuu alisema kabla ya ujenzi huo, inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya
madini ya Tanzanite yaliyokuwa
yanazalishwa kila mwaka, yalitoroshwa
kwa njia za panya na Serikali yetu haikuambulia chochote. “Hii ni
kutokana na kukosekana udhibiti wa kutosha wa madini ya tanzanite kuanzia kwenye uzalishaji hadi
kwa wauzaji,” alisema.
Alisema mbali na kuwepo kwa eneo la wachimbaji ndani ya ukuta wa Mererani, pia kutajengwa
maduka ya Tanzanite na viwanda vya kuongeza thamani, hususan vya
ukataji, uchongaji na ung’arishaji. Vilevile, kutakuwa na maeneo ya burudani ambayo
yatastawisha zaidi biashara ya Tanzanite
na kuwavuta watalii wengi kwenda kutembelea eneo hilo.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa reli
ya kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) itakayokuwa na urefu
wa km. 1,219 utarahisisha usafiri wa mizigo na
abiria na kuongeza itaongeza biashara hapa nchini pamoja na nchi za jirani.
Waziri Mkuu alisema mradi huo utakapokamilika, unatarajiwa kusafirisha tani
milioni 17 kwa mwaka, ikilinganishwa na tani milioni tano za sasa na kwamba utaongeza mapato kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kutunza barabara ambazo
zimekuwa zikiharibika mapema kutokana na kusafirisha mizigo mizito.
“Reli hii ya kisasa itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa takriban tani
10,000 kwa mara moja, ambayo ni sawa na malori (semi trailers) 500 yenye uwezo
wa kubeba tani 20 kila moja. Hii, itasaidia sio tu kutunza barabara zetu bali
pia kupunguza gharama za kukarabati barabara hizo mara kwa mara,” alisisitiza.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMANNE,
APRILI 10, 2018
No comments:
Post a Comment