WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema timu ya soka ya Namungo
ya Wilaya ya Ruangwa imepata udhamini wa sh. milioni 150 katika msimu ujao wa
ligi daraja la kwanza.
Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, ametoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Mei 25, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi
wa wilaya na mkoa mara baada kukagua uwanja mpya
unaojengwa katika kijiji cha
Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Amesema timu hiyo ambayo
imepanda daraja msimu huu wa ligi, imefanikiwa kupata mdhamini mkubwa ambaye ni
kampuni ya Haojue ya kutoka China inayouza pikipiki za aina ya SanLG.
“Bado tuko kwenye
mazungumzo na kampuni ya Uranex, hivi sasa wako mbioni kukamilisha taratibu za
udhamini, na wakikubali watakuwa wadhamini wetu namba mbili,” alisema.
Aliyataja makampuni na taasisi nyingine ambazo zimeshatoa
udhamini kwa timu hiyo kuwa ni Ngureme Co. Ltd (madini), Lindi Jumbo Ltd
(madini), Benki ya NMB, Halotel, CocaCola (ambao wametoa mipira 25 na jezi),
Mzee Bakhresa, kampuni ya AZAM, kampuni ya Nazareth, Masoud Jaba na Gemini
Exploring Ltd.
Alisema
hivi sasa kocha wa timu hiyo anaendelea na usajili wa wachezaji kwa ajili ya
msimu ujao, na tayari wachezaji 17 wamekwishasajiliwa, na wengine 10 bado
wanaendelea kufuatiliwa.
Waziri Mkuu aliishukuru kampuni ya Haojue kwa kukubali
kuidhamini timu hiyo. “Tuna uhakika kwamba wana-Namungo hawatalala njaa wakiwa
kambini,” alisema.
Kwa
upande wake, mshauri wa kampuni ya
Haojue hapa nchini, Bw. Martin Mbwana alisema wamekubali kuwa wadhamini wakuu kwa
gharama ya sh. milioni 150 kwa mwaka na udhamini wao utajumuisha jezi na viatu
vya wachezaji.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, MEI 26, 2018.
No comments:
Post a Comment