*Aagiza
Waziri wa Viwanda, RC na Menejimenti wakae na kumpa taarifa leo jioni
*Asema
tofauti ya viwango vya mishahara inatisha, ataka orodha ya watumishi
*Awataka
watumishi walioko kazini, likizo wawe wastahimilivu
SERIKALI imesema hairidhiki na ubia unaoendeshwa kwenye Kiwanda cha Nguo
cha Urafiki.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo jioni (Ijumaa, Juni
mosi, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wafanyakazi wa kiwanda hicho mara
baada ya kukagua mitambo mbalimbali kwenye kiwanda hicho.
“Serikali haturidhiki na ubia huu, na huyu mbia
aelewe kwamba Serikali haturidhishwi na ubia huu wala kinachoendelea hapa kiwandani,”
amesema huku akishangiliwa kwa nguvu na wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles
Mwijage aongoze kikao baina ya wabia hao na menejimenti ya kiwanda na apewe
taarifa hiyo leo saa 12 jioni baada ya kufuturu.
“Ubia wenu hauna tija. Kwa hiyo wewe Msajili wa Hazina na huyo mwekezaji,
nikitoka hapa, mbaki mfanye kikao na mnipe majibu leo saa 12 jioni. Mheshimiwa Waziri
wa Viwanda na Mkuu wa Mkoa muongoze mjadala huo na nikitoka kufuturu mniambie
maazimio yenu, na kama haiwezekani, mvunje kabisa ubia huo ili tujue hatuna mbia
tutafute mbia,” amesema.
Waziri Mkuu amesema wabia wakuu wa kiwanda hicho ni Msajili wa Hazina na
kampuni ya Changzhou State owned Textile
Assets Operations kutoka China na kwamba Serikali ilipoamua kukaribisha uwekezaji
ilitarajia kupata mtaji, teknolojia na ajira za kutosha lakini hali ya sasa ni
kinyume kabisa.
“Hatuwezi kuvumilia, tunasema tuna mbia mwenye mtaji, hakuna mtaji;
tulisema tunataka mbia mwenye kuleta teknolojia mpya, hakuna teknolojia;
tulisema aendeshe shughuli hii kukiwa na ajira endelevu, hizo ajira hakuna;
halafu tubaki tunamwangalia tu. Bora atuambie amekwama, aondoke, tutangaze
vinginevyo,” amesema.
“Tulikopa mtaji lakini Tanzania hizo hela hazijaja, tunataka majibu ya
fedha hizo; kama fedha iliyokopwa kwenye Benki ya Exim ya China ingeletwa
nchini tungeweza kuziba mapengo na kusaidia kiwanda kiweze kufanya kazi. Sasa
kwa sababu fedha hiyo haijaja nchini, tunataka maelezo fedha hiyo iko wapi?” amesisitiza.
“Mitambo iliyonunuliwa na mwekezaji miaka mitano au sita iliyopita
haifanyi kazi tangu ilipoletwa nchini, nataka majibu, je mitambo hii
ilinunuliwa ikiwa mizima au vipi; na tena mmeng’oa mashine kwenye ma-godown
matatu, nimeambiwa mlikuwa na nia ya kuleta mashine mpya, lakini sasa ni miaka
mitano, je mashine zile zote zimeenda wapi, na kama mmeuza ameuziwa nani? Mkae mjadili
na leo hii mniletee majibu yote haya,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema kiwanda hicho ni matokeo ya urafiki wa China na Tanzania
na kina historia ndefu na mahusiano ya muda mrefu. “Asiingie mtu akatuharibia, na
tunataka mahusiano yetu na China yaendelee. Amesema baada ya kupokea taarifa
hiyo, Serikali itakaa na Balozi wa China ili itafutwe suluhisho.
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa kiwanda hicho walioko likizo na wale
waliopo kazini wawe wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta dawa ya
matatizo yao.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemtaka Meneja Rasilmali Watu na Utawala wa kiwanda
hicho, Bw. Edwin Nkwanga aandae orodha ya watumishi wote yenye kuonyesha kila
mtumishi analipwa nini na aifikishe kwake haraka.
“Hapa kuna watu wanalipwa sh. milioni saba hadi 10 na wengine wanalipwa
sh. 120,000. Niletee orodha yenye kuonyesha jina, cheo na kiwango cha mshahara,
lakini pia uonyeshe anapata stahili zipi, kama ni posho ya nyumba, maji au
umeme,” amesema.
Amesema nia ya Serikali ni kutaka kupanga upya mishahara yao ili waweze
kupatikana watumishi wa kutosha.
Wakati akikagua
kiwanda hicho, Waziri Mkuu alielezwa
kwamba kuna mashine 88 ambazo ziling’olewa kwenye kiwanda hicho na
hazijulikani zimepelekwa wapi.
Mapema, akitoa taarifa fupi ya kiwanda hicho, Naibu Meneja Mkuu wa kiwanda
hicho, Bw. Shadrack Nkelebe alisema kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji
tangu Desemba 2017 ili kufanya ukarabati na kimeshindwa kuendelea nao kwa
sababu ya madeni.
“Kiwanda kilikuwa na watumishi 3,000 lakini sasa hivi wamebakia 726 baada
ya wengine kupunguzwa na kulazimishwa kwenda likizo licha ya teknolojia kubakia
ni ileile. Kiwanda kinakabiliwa na changamoto nyingi lakini kwa sehemu kubwa ni
za kutengeneza. Tumepigana vita katika kujenga uchumi wa Taifa kupitia kiwanda
hiki, lakini tumekwama. Tunahitaji nguvu ya ziada ili tutoke hapa,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
IJUMAA, JUNI
MOSI, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Naibu Meneja
Mkuu wa kiwanda cha nguo cha Urafiki, Shadrack Nkelebe kuhusu mashine za
kutengeneza nyuzi za pamba wakati alipokitembelea kiwanda hicho, Juni
1, 2018. Kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji tangu Desemba mwaka
jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipita katika eneo zilipong'olewa mashine za kiwanda cha nguo cha
Urafiki cha jijini Dar es salaam wakati alipotembelea kiwanda hicho Juni
1, 2018. Kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji tangu Desemba mwaka
jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipita katika eneo zilipong'olewa mashine za kiwanda cha nguo cha
Urafiki cha jijini Dar es salaam wakati alipotembelea kiwanda hicho Juni
1, 2018. Kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji tangu Desemba mwaka
jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipita katika eneo zilipong'olewa mashine za kiwanda cha nguo cha
Urafiki cha jijini Dar es salaam wakati alipotembelea kiwanda hicho Juni
1, 2018. Kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji tangu Desemba mwaka
jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mhandisi
Mkuu wa kiwanda cha nguo cha Urafiki cha jijini Dar es salaam, Khamis
Mazugo (kushoto) kuhusu mitambo ya kiwanda hicho iliyokoma kufanya kazi
wakati alipotembelea kiwanda hicho Juni 1, 2018. Kiwanda hicho
kimesimamisha uzalishaji tangu Desemba mwaka jana.(Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akizungumza na wafanyakazi na viongozi wa kiwanda cha nguo cha
Urafiki cha jijini Dar es salaam baada ya kukagua kiwanda hicho Juni 1,
2018. Kushoto ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage na kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Mkuu wa Mkoa
wa Pwani, Mhandisi, Evarest Ndikilo. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment