WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage, amewataka
wahandisi nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji katika viwanda nchini ili
kuiwezesha Serikali kufikia lengo la uchumi wa kati na jumuishi ifikapo 2025.
Mwijage alisema hayo
jana wakati akifungua kongamano la siku moja la wahandisi kuhusu mchango wa wahandisi
katika sekta ya viwanda jijini Dodoma.
Alisema mchango wa
wahandisi ni muhimu sana katika kipindi hiki ili kuwezesha taifa kufikia uchumi
wa kati wenye uwiano kati ya pato la nchi na uchumi wa mwananchi.
“Tumejipanga kuanzisha
viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini ili kuongeza thamani
ya mazao ya kilimo na hivyo kugusa uchumi wa wananchi wengi” alisema Mwijage.
Alisema uwekezaji
katika viwanda vya sukari, mafuta na vifaa vya ujenzi ambavyo vyote malighafi
zake zinapatikana nchini, utawezesha idadi kubwa ya wananchi wa Tanzania kupata
ajira na hivyo kufikia lengo la Taifa la
uchumi wa kipato cha kati.
Naye Mwenyekiti wa Bodi
ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), Mhandisi Profesa Ninatubu Lema ameiomba
Serikali kuthubutu kuwaamini wahandisi wazalendo kusimamia
na kutekeleza miradi
mikubwa ya ujenzi hapa nchini.
Prof. Lema alisema
wahandisi wako tayari hata kupewa sehemu kidogo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa ya (Standard
Gauge), ili nao waweke alama ya uzalendo katika mradi huo mkubwa unaotekelezwa
nchini.
“Tunapoadhimisha miaka
50 ya ERB tuko wahandisi tuliosajiliwa zaidi ya elfu 21 tunaweza kufanya kitu
kama alama kwa taifa na vizazi vijavyo”,
alisema Lema.
Amewataka wahandisi
kutathmini namna gani wanaweza kuendeleza kilimo na viwanda nchini ili kuweza
kubadili uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla katika miaka ijayo.
Kaimu Msajili wa ERB, Mhandisi
Patrick Barozi, alisema kongamano la wahandisi kuhusu uchumi wa viwanda ni
sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Bodi ya wahandisi yanayofanyika katika
sekta mbalimbali za kihandisi yatakayofikia kilele chake mwezi Septemba mwaka
huu.
Alisema lengo la
kongamano hilo ni kuwakutanisha wahandisi pamoja kutafakari na kuhamasishana
kuhusu namna bora ya kuendeleleza taaluma ya uhandisi kukuza uchumi wa nchi na
wa mtu mmoja mmoja.
No comments:
Post a Comment