HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 23, 2018

KIGOGO YANGA AJIUZULU


Na Mwandishi Wetu

HATIMAYE aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga leo ametangaza rasmi kujiweka kando na uongozi wa klabu hiyo baada ya mashabiki wa klabu hiyo kumtishia maisha yeye na familia yake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam, Sanga alisema tishio la maisha yake linaloihusu pia familia yake lilitolewa Ijumaa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari.

Sanga alisema kilichomsukuma kuchukua uamuzi huo ni vitisho na si majukumu ya kazi yake ambayo yanaweza kuvumilika lakini suala la kutishiana maisha hawezi kulivumilia ingawa ni shabiki na mpenzi mkubwa wa soka.

“Mara nyingi kumejitokeza taarifa kuhusu kutishiwa kwangu maisha kwa ajili ya nafasi ninayoiongoza, nimetangaza kujiuzulu rasmi ingawa uongozi wetu ulitakiwa kufikia tamati mwaka 2020 lakini kwa aina hii ya vitisho ambavyo sio utamaduni wetu, najiuzulu rasmi nafasi yangu.

Sanga alisema amesitushwa na taarifa hizo ambazo, wadau hao wamehamasishana kwa kila shabiki wa timu hiyo kwenda nyumbani kwake akiwa na panga, shoka na vifaa vingine ili kumuamuru aachie madaraka katika timu hiyo.

Pamoja na kutaka kwenda nyumbani kwake na zana hizo za kilimo, pia nimeshangazwa na huyo mtu aliyefikia hatua ya kumuomba Rais John Magufuli anishughulikie mimi kwa sababu naonekana nipo juu ya serikali wakati sivyo hivyo mimi ni mtu wa kawaida.
 
“Nilishangazwa taarifa ile iliyohamasisha mashabiki na wapenzi wa Yanga mwenye Panga, Shoka, Jembe na vinginevyo nilidhani labda nyumbani kwangu kuna shamba ambalo wana Yanga wanataka kunisaidia kulima, lakini nashangaa wadau wengi hawalikemei suala hilo ambalo nalifananisha na matembele yanayotambaa,” alisema Sanga.

Sanga alisema kupitia vitisho hivyo alitegemea vyombo vinavyohusika na masuala ya usalama kwani sio utamaduni wa Tanzania kutishiana maisha, hivyo anauona kama ni utamaduni na kueleza kwamba kujiweka kwake pembeni ni kuona kama chuki hiyo itaendelea ama la.

“Naachia ngazi Yanga lakini nashukuru wanachama na wapenzi wa soka sambamba na Bodi ya Ligi (TPLB) timu naicha kwa Baraza la Wadhamini ambalo ndilo linalinda mali ya klabu.   

Alitumia fursa hiyo kuelezea kuenguliwa kwake katika bodi ya Ligi (TPLB) kwamba anashangazwa na hatua iliyochukuliwa na kwamba kabla ya uchaguzi taratibu zote zilifanyika ndio maana akawa Mwenyekiti wa bodi. 

Kujiuzulu kwa Sanga kumekuja siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa kujiuzulu nafasi yake akitoa sababu za kiafya, Kaimu Mwenyekiti wa timu hiyo, Clement Sanga naye amefuata nyayo hizo jana.
Hiyo ni mwaka mmoja tangu Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ajiuzulu huku wanachama wakigoma kutambua kujiuzulu kwake.

Manji na Katibu Mkuu wa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Yanga Mkwasa wamejiuzulu kwa sababu za kiafya ila nitofauti kwa Sanga ambaye inaelezwa ameshinikizwa na wanachama wa timu hiyo kupitia vitisho vilivyotolewa na baadhi ya wanachama.

Baada ya kuondoka Manji, alifuata mjumbe wa Kamati Tendaji Salum Mkemi miezi michache iliyopita, kisha akafuata Abbas Tarimba, ambaye inadaiwa amerejea, kisha Abdallah Bin Kleb na baadaye akaja Mkwasa, huku juzi akijiondoa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano, Khalfani Hamisi.

Wakati sintofahamu ya nafasi za watendaji hao ikionekana kuumiza vichwa vya mashabiki na wanachama, juzi kuliibuka tetesi kuwa Ofisa Habari, Dismas Ten naye anatembea na barua ya kuacha kazi ndani ya kikosi hicho.

Manji, Mkwasa na Bin Kleb wamejiuzulu kwa sababu za kiafya, Mkemi akikiriri kushindwa, huku mjumbe huyo aliyejiuzulu hivi karibuni akieleza kuwa tatizo ni mwenendo mbaya wa timu yao pamoja na Makamu Mwenyekiti wao, Sanga anayeonekana hana msaada katika kikosi hicho.

Kujiuzulu kwa Manji kumeiweka Yanga katika mdororo wa kiuchumi unaosababisha klabu kushindwa kujiendesha kwa ufanisi kiasi cha kutoweza kufanya usajili wa nyota wakubwa ikiwemo kukosa nguvu za kusaini mikataba mipya ya wachezaji wao nyota waliomaliza kandarasi zao.

Wakati hali ikiwa hivyo, Mkwasa aliyeanza kuitumikia Yanga kama mchezaji miaka ya 1980, baadaye kocha kuanzia miaka ya 1999 kabla ya kuingia kwenye uongozi miaka miwili iliyopita, akafuata kujiuzulu.

Kutoka kwa Mkwasa, kumeonekana kama kufungua njia kwa wengine ambao wameanza kujiengua akiwemo, Khalfan ambaye aliteuliwa Juni mwaka jana katika kamati hiyo uliyoundwa na watu 26.

Tukio alilofanyiwa Sanga kwa Yanga sio la kwanza kwani aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga aliyevamiwa nyumbani kwake saa nane usiku na kutishiwa maisha na wanachama wa Yanga na kusababisha Mei 24, 2012 mwanasheria huyo kutangaza kuachia ngazi kuiongoza timu hiyo.

Kilichosababisha Nchunga kuachia madaraka hayo kilitokana na kipigo cha mabao 5-0 ilichokipata Yanga kutoka kwa watani zake Simba, mchezo uliochezwa Mei 6, 2012 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi aliyefunga mawili, Felix Sunzu. Patrick Mafisango na Kipa Juma Kaseja.

Mzee Akilimali aitaka Yanga Kampuni
Kutokana na sintofahamu inayoendelea katika klabu ya Young Africans Mjumbe wa Baraza la Wazee wa klabu hiyo Mzee Ibrahim Akilimali ameibuka na kutaka Yanga Kampuni ambayo itakuwa suluhisho la matatizo klabuni hapo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili Mzee Akilimali alisema migogoro inayojitokeza sasa ni kutokana na kushindwa kuweka mfumo sahihi wa uendeshaji uliopendekezwa miaka ya nyuma.

"Manji akatufundisha klabu yoyote kwa muda huu haiwezi kwenda vizuri ila ni lazima hii inayoitwa Yanga Kampuni ibadilishwe na kuwa kampuni ya umma," alisema Akilimali.
Aidha Mzee Akilimali aliongeza kuwa kampuni hiyo ikishabadilishwa na kuwa ya umma hisa itakuwa asilimia 51 ya klabu 49 ya wawekezaji wengine ili kuweza kuhimili changamoto mbalimbali. 

Katibu Mkuu wa zamani wa klabu hiyo George Mpondela (marehemu), ndiye aliyeanzisha wazo la Yanga Kampuni ambalo lingekuwa dawa ya wafadhili wanaojiondoa ghafla na kuiacha klabu ikisuasua.

Wazo la Mpondela lilipokelewa vema na washirika wengine akiwamo Abbas Tarimba walipita kuwaelemisha wanachama hatimaye chini ya mwanachama Yusuf Mzimba kuliibuka mgogoro wa Yanga Asili na Yanga Kampuni.

Wakati huohuo, Mfadhili wa Simba, Mohamed Dewji Mo amesikitishwa na mwenendo mbaya unaowatetemesha watani zao hao ambao hivi sasa klabu hiyo kongwe inapitia katika kipindi kigumu.

“Tunahitaji Yanga imara ambayo inaweza kushindana na Simba. Tunahitaji Yanga imara kwa ajili ya timu bora ya Taifa ya Tanzania. Ninawaombea Yanga waweze kupita katika kipindi hiki kigumu kwao, wanapaswa watulie na waungane upya,” alisema Mo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

No comments:

Post a Comment

Pages