*Asema
sanaa inaweza kutumika kuondoa umaskini
*Atamani
Watanzania wauenzi utamaduni kama Wachina
WAZIRI
MKUU mstaafu Mizengo Pinda amesema tasnia ya sanaa ina nafasi kubwa ya kuweza
kuondoa umaskini katika ngazi zote kama itatumiwa vizuri.
Ametoa
kauli hiyo mwishoni mwa wiki nyumbani kwake Nzinje, nje kidogo ya Jiji la Dodoma,
wakati alipokutana na wawakilishi wa Mradi wa Utambuzi wa Sanaa za Ufundi
Tanzania (TACIP) waliokwenda kumuomba awe mlezi (champion) wa mradi huo.
“Tasnia
ya sanaa ni nafasi kubwa ya ajabu ya kuondoa umaskini katika ngazi zote kama
tutaitumia vizuri. Nimepokea heshima hii ya kuwa mlezi wa TACIP na naahidi kuwa
sitawaangusha,” alisema.
Alisema wiki iliyopita, alipata
bahati ya kukutana na viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) jijini Dodoma
na alichobaini ni kwamba katika kila eneo walilojadili, walikuwa wakihusisha na
suala la sanaa na utamaduni na jinsi inavyoweza kutumika kama njia ya kutoa
suluhisho ya tatizo liliopo.
“Wenzetu wako makini sana na kutunza
utamaduni wao, lolote atakalojadili lazima aweke umuhimu wa sanaa na utamaduni
wao. Wenzetu wameona utamduni ni zana ya kutatua tatizo lolote linaloizunguka
jamii yao,” alisema.
“Kwa mfano, katika kukabiliana na
tatizo la mazingira, wametumia wasanii kupeleka ujumbe wa kuelezea maovu dhidi
ya mazingira na mambo mazuri yanayodumisha mazingira. Katika elimu wametumia
sanaa. Kwangu mimi natamani tubaini ni mambo gani tunaweza kujifunza kutoka kwa
Wachina katika kukuza sanaa,” alisema.
Alisema kwa Tanzania hali ni
tofauti kwa sababu wasanii bado wanatumika kwa ajili ya kutoa burudani tu. “Huku
kwetu wasanii wanatumika kutoa burudani, inabidi tubadilishe mtazamo huu kwa
kushirikiana na Serikali kupeleka ujumbe huu mpya,” alisema.
Alikiri kuwa tasnia ya sanaa ina
washiriki zaidi ya milioni sita ambao hawajawahi kuunganishwa na chombo maalum
na kwamba kuanzishwa kwa TACIP kutaleta ukombozi kwenye sekta hiyo muhimu kwa
Taifa.
Mapema, Mratibu wa mradi huo, Bw. Macmillan George alimweleza Mhe. Pinda kwamba mradi
umepangwa kutekelezwa kwenye kanda sita ambazo ni Pwani Mashariki, Nyanda za
Juu Kusini, Kaskazini na Magharibi. Nyingine ni kanda ya Kati na kanda ya Ziwa.
Alisema wiki ijayo wanatarajia
kuanza kukusanya taarifa za wasanii wa sanaa za ufundi kwa kuanza na mkoa wa
Dar es Salaam. Wasanii hao wanajumuisha wachoraji, wachongaji (sculptors), wanasanaa
za mikono (crafts), wanasanaa jumuishi (peripheral artists), wafinyanzi (ceramics)
na wabunifu (designers).
Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Bw. Nicholaus William ambaye aliambatana na viongozi hao, alisema
Serikali inaubeba mradi huo kwa uzito mkubwa.
Alisema kuwepo kwa mradi huo
kunatarajiwa kutatua changamoto za wasanii nchini ambazo zimedumu kwa muda
mrefu. Kaulimbiu ya mradi huo ni: “Jitambue, Tambulika, Inalipa.”
Mradi wa TACIP (Tanzania
Arts and Crafts Identification Project) ambao unatekelezwa kwa ubia kati ya Tanzania
Arts and Crafts Identification Project (TAFCA) na DataVision International umelenga
kuiwezesha sekta ya sanaa za ufundi Tanzania Bara kuwaongezea kipato washiriki
wake, hususan katika kujikwamua kutoka kwenye balaa la umasikini na kuwawezesha
kuchangia pato la Taifa.
Mradi
huo pia umelenga kuwatambua washiriki wa sekta hiyo na kuwapatia vitambulisho
vya kisasa vya kieletroniki; kuanzisha tovuti maalumu ya wasanii hao yenye
taarifa za majina, jinsi, umri, mahali walipo na wanachozalisha; kufungua
tovuti ya e-commerce portal ili kuwezesha biashara mtandao ya kazi za sanaa za
ufundi; kuwahamasisha wajisajili kisheria na kujiunga katika vikundi na vyama
ili wawe na nguvu ya sauti na waweze kukubalika kukopa katika taasisi za fedha.
IMETOLEWA:
DODOMA,
JUMAPILI, JULAI MOSI, 2018.
Mratibu
wa Mradi
wa Utambuzi wa Sanaa za Ufundi Tanzania (TACIP), Bw. Macmillan George akimsikiliza
Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda wakati akielezea umuhimu wa kutumia
sanaa kupeleka ujumbe kwa jamii.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe.
Mizengo Pinda akielezea jambo kwa wawakilishi wa mradi wa TACIP baada ya kupokea barua yao. Kushoto
ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Nicholaus William na katikati ni Mratibu wa
mradi huo, Bw. Macmillan George.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe.
Mizengo Pinda akiongea na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Nicholaus
William baada ya kupokea zawadi ya picha ya kuchora ya simba iliyotolewa na
wawakilishi wa mradi wa TACIP.
Waziri
Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda akimsikiliza Rais wa TAFCA na Mtendaji
Mkuu Mshirika wa Mradi wa Utambuzi wa Sanaa za Ufundi Tanzania (TACIP), Bw.
Adrian Nyangamalle wakati yeye na wenzake walipomtembelea nyumbani kwake,
kijiji cha Nzinje, nje kidogo ya Jiji la Dodoma kumuomba awe mlezi wa mradi
huo.
Wawakilishi
wa mradi wa TACIP wakiwa katika
picha ya pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda (wa
pili kushoto) mara baada ya kuwasilisha barua yao kumuomba awe mlezi wa mradi
huo. Wengine kutoka kulia, walioko mstari wa mbele ni Mshauri wa mradi huo,
Mzee Rashid Masimbi, Naibu Katibu Mkuu wa HUSM, Bw. Nicholaus William na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi
wa TEHAMA wa DataVision International, Dk. Shaaban Kiwanga.
No comments:
Post a Comment