HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 01, 2018

AJALI YA GARI YAUA WATU 20 JIJINI MBEYA, RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Baadhi ya wananchi jijini Mbeya wakiangalia lori lililogonga daladala tatu leo na kusababisha vifo vya watu 20.


“Nimesikitishwa sana na taarifa ya ajali nyingine iliyotokea leo tarehe 01 Julai, 2018 katika mteremko wa Iwambi Mkoani Mbeya na kusababisha vifo vya Watanzania wenzetu 20, hii ni ajali ya tatu kutokea Mbeya katika kipindi kifupi ambapo katika ajali hizo idadi ya Watanzania waliopoteza maisha imefikia 40.

“Inauma sana kuwapoteza idadi hii kubwa ya Watanzania wenzetu katika ajali za barabarani ambazo tunaweza kuziepuka. Nawapa pole familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo vya Watanzania wenzetu hawa, sote tuwaombee Marehemu wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wapone haraka”

Ni salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozitoa leo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Amos Makalla kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha watu 20 kufariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa baada ya Lori (Semi-Trailer) kuyagonga mabasi madogo ya abiria 3 likiwemo 1 lililolaliwa na tela lenye kontena baada ya kugongwa na kutumbukia mtoni katika eneo la Iwambi, Mkoani Mbeya.
Katika ajali hiyo Lori lililokuwa limebeba kontena lenye shehena ya mzigo, lilikuwa linatokea Mbeya Mjini kwenda Tunduma (katika barabara ya Dar es Salaam – Tunduma – Zambia) na mabasi madogo ya abiria (Daladala) ni yanayofanya safari zake kati Mwanjelwa na Mbalizi.
Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wa Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi na Mamlaka nyingine zinazohusika katika udhibiti wa usalama wa barabarani kujifakari na kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na ajali hizo.
“Haikubaliki hata kidogo kuendelea kupoteza roho za watu katika ajali tunazoweza kuzizuia” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Julai, 2018

No comments:

Post a Comment

Pages