Kufuatia Ofisi ya Rais, TAMISEMI
kuwapangia jumla ya walimu 4,840 vituo vya kazi kwenye Shule za Msingi na
Sekondari nchini, Katibu Ofisi ya Rais,
Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutaindurwa amewataka waajiriwa hao kuzingatia
kanuni na taratibu zinazosimamia utumishi wa walimu ili kujiepusha na makosa ya
kinidhamu.
Amesema kuwa, kumekuwa na mazoea
kwa walimu wengi kusaini nyaraka wanazopewa wakati wa kuanza ajira bila kuzisoma kitu
kinachosababisha kutoelewa kanuni na taratibu za taaluma ya ualimu katika
utumishi wa Umma.
“Wapo walimu wengi ambao wamechukuliwa hatua
mbalimbali za kinidhamu na wengine wamejikuta wakipoteza ajira zao kwa sababu
ya kwenda kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu pamoja na
zile zinazoongoza Utumishi wa Umma” amesema Bibi Rutaindurwa.
Amefafanua kuwa, Mwajiriwa atakaporipoti
kwenye Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya yenye Shule aliyopangiwa, atapewa mkataba wa ajira
ulioandaliwa na Tume ya Utumishi wa Walimu. Mwajiriwa anatakiwa kusoma mkataba
huo pamoja na viambatisho vyake ili
aweze kujua haki na wajibu katika utumishi wake.
“Mara nyingi walimu wanapoajiriwa, wengi wao wanasaini mikataba ya ajira bila kuisoma
na kuelewa. Sasa naelekeza kuwa, kila
Mwalimu ahakikishe anasoma mkataba wake na anauelewa vizuri kabla hajausaini
ili kujua kwa undani kile anachotakiwa
kufanya katika utumishi wake” amesema Bibi Rutaindurwa.
Ameongeza kuwa, waajiriwa
wanapaswa kusoma Sheria ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2015, Kanuni pamoja na Miongozo
mingine ambayo inapatikana katika tovuti ya Tume ya Utumishi wa Walimu kupitia www.tsc.go.tz.
Wakati huo huo, Bibi Rutaindurwa amewataka
Kaimu Katibu Wasaidizi Wilaya zote kuhakikisha wanatoa ufafanuzi wa mikataba
pamoja na kuwaelimisha walimu walioajiriwa masuala mbalimbali yanayohusu ajira
zao kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu na. 25 ya mwaka 2015.
Ameelekeza kuwa, baada ya mwalimu
kukamilisha taratibu zote za kiutumishi,
Kaimu Katibu Wasaidizi watoe barua za ajira kwa waajiriwa wapya kwa
wakati bila kuweka urasimu unaoleta usumbufu.
Ameongeza kuwa, hatamvumila Mtendaji
yeyote wa Tume ya Utumishi wa Walimu ambaye atafanya uzembe au kuchelewesha
barua za ajira kwa Walimu bila sababu za
msingi.
“Mwalimu anapokamilisha kujaza
nyaraka za ajira yake apewe barua ya ajira, bila urasimu wowote ili aanze
kutekeleza majukumu yake kwa haraka. Sitaki kusikia mwalimu amechelewa kupata
barua ya ajira au kuna mtumishi wa Tume analeta urasimu kinyume na taratibu,
kwa kweli sitamvumilia” amesema Bibi Rutaindurwa.
Vilevile, amewakumbusha Walimu
Wakuu na Wakuu wa Shule kuwashauri na
kuwaelimisha walimu juu ya kanuni na taratibu za kiutumishi badala ya kukaa na
kusubiri wafanye makosa ili wawachukulie hatua za kinidhamu.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2015, Walimu
Wakuu na Wakuu wa Shule ndio mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa mwalimu. Hivyo,
walimu wanapaswa kuzingatia matakwa ya Sheria na Kanuni za Utumishi wa Walimu
na zile za Utumishi wa Umma.
Adili
Mhina,
Afisa Mawasiliano,
Tume ya Utumishi
wa Walimu.
22/07/2018.
No comments:
Post a Comment