WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo rasmi ya kiserikali na mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon ambaye yuko hapa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Viongozi
hao wawili, kwa pamoja, leo mchana (Jumapili, Julai 22, 2018)
wameshuhudia uwekaji saini mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa watu
wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi (diplomatic and
service passports).
Uwekaji
saini huo ulifanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga na Makamu wa Kwanza Wizara ya Mambo ya
Nje wa Jamhuri ya Korea, Bw. Lim Sung-nam kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na waandishi wa habari waliohudhuria hafla ya uwekaji saini, Waziri
Mkuu amesema kwenye mazungumzo yao wamejadiliana mambo mengi ambayo
yamelenga kukuza uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
“Tumejadili namna ya kuimarisha mahusiano yetu kidiplomasia; kuimarisha ushirikiano
katika sekta ya uchumi na maendeleo; ushirikiano katika elimu, sayansi
na TEHAMA ushirikiano katika sekta ya utamaduni na utalii,” amesema.
“Pia
tumeongelea fursa ya mradi mkubwa wa reli, ujenzi wa daraja la
Salender, mradi wa hospitali ya Mloganzila; mradi wa NIDA ambao tumepata
mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kuendelea kutoa vitambulisho vya
uraia; ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi lenye urefu wa mita 3,200;
ujenzi wa barabara ya Kazirambwa – Chaya yenye urefu wa km. 42 na
uimarishaji wa sekta ya afya kwa kujenga hospitali tano za rufaa kwenye
kanda zetu,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema amewaalika makampuni ya kutoka Jamhuri ya Korea yaje
kuwekeza nchini ili kuiwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa nchi
ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. “Pia wafanyabiashara aliokuja
nao, kesho watashiriki kongamano la kibiashara baina ya Korea na
Tanzania ili waweze kubadilishana uzoefu na wenzao wa Tanzania.”
“Tumewaomba
pia watangaze vivutio vya utalii vya hapa nchini huko kwao na Balozi
wetu wa Tanzania huko Korea atasimamia utangazaji wa vivutio vya hapa
nchini kwetu. Sisi pia tumewapongeza kwa uamuzi wa Korea Kusini kukaa
pamoja na Korea Kaskazini na kuimarisha amani kwa nchi zao,” amesema.
Mkutano
huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng.
Isack Kamwele; Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani; Waziri wa
Viwanda na Biashara wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ally; Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Bw. Issa Gavu na Naibu Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya. Wengine ni Makatibu Wakuu
wa wizara mbalimbali na wakuu wa taasisi.
Waziri
Mkuu Lee Nak-yon anatembelea Tanzania ikiwa ni hatua ya kuimarisha
uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Hii ni mara ya kwanza
kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara ya kiserikali
tangu nchi hizo zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.
Jamhuri
ya Korea ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo
kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo (KOICA) na Mfuko wa
Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo (EDCF) yamekuwa yakitoa misaada na
mikopo ya masharti nafuu ikiwemo misaada ya fedha katika bajeti, ujenzi
wa miundombinu ya jamii, mafunzo ya muda mfupi na mrefu, wataalamu wa
kujitolea, vifaa na mashine kwa ajili ya sekta mbalimbali ikiwemo ya
afya.
Baadhi
ya miradi ambayo imegharamiwa na Serikali ya Korea ni pamoja na Mradi
wa kuboresha Huduma ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Chanika, Mradi
wa Mfumo wa Usajili wa Meli na Mabaharia kwa Njia ya Mtandao Zanzibar,
Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Taaluma na Tiba (MUHAS) kampasi
ya Mloganzila na ujenzi wa daraja katika mto Malagarasi.
Vile
vile, Korea ni mshirika mkubwa katika kusaidia maendeleo ya Bara la
Afrika ambapo hivi karibuni katika mkutano wa Sita wa Jukwaa la
Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Afrika (KOAFEC VI) uliofanyika
Mei 2018, Busan, Korea ambapo Serikali ya Korea ilitangaza msaada wa
dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya Bara la Afrika kwa kipindi cha
2018-2020. Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na msaada huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 22, 2018.
No comments:
Post a Comment