*Aalika wawekezaji kwenye viwanda vya kuongeza
thamani ya mazao
*Ataka waangalie fursa za uwekezaji zilizopo kwenye
sekta ya utalii
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaalika wafanyabiashara kutoka Korea Kusini waanzishe miradi ya uwekezaji kwenye
sekta ya viwanda kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani.
Ametoa mwaliko huo leo (Jumatatu,
Julai 23, 2018) akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon wakati akifungua Kongamano
la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Korea lililofanyika kwenye
hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Kongamano la kwanza lilifanyika jijini Seoul,
Februari 2018.
Amesema Serikali
inahamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vinavyotumia rasilimali za
ndani ambavyo vitasaidia kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo, misitu,
madini na bahari.
“Tunakaribisha uwekezaji wa
viwanda katika maeneo ya uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za walaji
(consumer goods), pamoja na viwanda vya kuunganisha bidhaa mbalimbali, yaani
(assembling plants) kama vile magari, simu na majokofu,” amesema.
Waziri Mkuu pia aliwaalika
wafanyabiashara kutoka Korea waliohudhuria kongamano hilo waje kuwekeza kwenye
sekta ya utalii ambako alisema kuna vivutio vya mbuga za wanyama kama
Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Olduvai Gorge na fukwe za bahari za Tanzania bara
na Zanzibar.
“Tanzania ina kilometa 1,200
za fukwe kuanzia Tanga hadi Mtwara, ziko pia fukwe za Zanzibar, ziko fukwe kwenye
maziwa yetu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ambazo ni kivutio kingine cha
utalii,” amesema.
Amesema ili kusimamia
matumizi ya fukwe hizo, Serikali inakamilisha uundaji wa Mamlaka ya Usimamizi
wa Fukwe kama ilivyo ile ya Ngorongoro ambayo alisema taratibu zikikamilika, itaanza
kazi hivi karibuni.
Kwa
upande wake,
Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Lee Nak-yon aliwapongeza viongozi wa Serikali ya Tanzania
kwa kufanikisha mageuzi ya kiuchumi hadi kuiwezesha nchi hii kuwa mojawapo ya
nchi 10 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa haraka.
“Mapema mwaka huu,
Benki ya Dunia imeitambua Tanzania na kuitangaza kuwa ni miongoni mwa nchi 10
ambazo uchumi wake unakua kwa haraka duniani. Nitumie nafasi hii kuwapongeza
viongozi wa Serikali hii pamoja na wafanyabiashara na wajasiriamali wa nchi
hii,” alisema.
Alitumia fursa hiyo
kuwaeleza wafanyabiashara na wenye makampuni kutoka Korea ambao wanashiriki
kongamano hilo kwamba amepokea maombi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ambaye ameyaalika makampuni ya Kikorea yashiriki
kwenye miradi mikubwa ya uwekezaji.
“Ukiondoa mradi wa ujenzi wa
daraja la Salender ambao mkataba wake umesainiwa leo, Rais Magufuli ameomba
makampuni ya Kikorea yashiriki kwenye miradi mikubwa ya kiuchumi na hivi
karibuni, taratibu zikikamilika, kuna kampuni moja itasaini mkataba wa kujenga
meli kubwa kwenye Ziwa Victoria, na siyo huko tu, hata kwenye Ziwa Tanganyika,”
alisema.
Alieleza kuridhishwa kwake
na ujenzi unaofanywa kwenye miradi ya kituo cha data cha NIDA (Kibaha) na mradi
wa kuboresha huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo aliitembelea
jana jioni.
Waziri Mkuu wa Korea Kusini
anatarajiwa kuondoka nchini leo jioni (Julai 23, 2018).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI
23, 2018.
No comments:
Post a Comment