Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akipewa maelezo ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Kiganamo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mkoani Kigoma, kutoka kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Mshana Dastan, alipotembelea na kufanya ukaguzi wa Kituo hicho.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akikagua wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Kiganamo
Wilayani Kasulu, Mkoani Kigoma akiwa
katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali iliyopewa fedha na Hazina. (Picha na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango).
Benny Mwaipaja, Kasulu,
Kigoma
Serikali imepanga kujenga
zaidi ya vituo 120 vya afya nchini kote katika mwaka wa fedha 2018/19 ili kusogeza
huduma za afya karibu zaidi na wananchi ikiwemo huduma ya mama na mtoto.
Hayo yamesemwa Mjini
Kasulu, mkoani Kigoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alipotembelea
na kukagua ujenzi wa majengo mapya ya Kituo cha Afya Kiganamo, yaliyo gharimu
shilingi milioni 500.
Amesema kuwa tangu
Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani imeongeza bajeti ya Wizara ya Afya
kutoka shilingi bilioni 30 hadi kufikia shilingi bilioni 369, hatua iliyolenga
kuboresha afya za wananchi kwa kuwa hakuna maendeleo kama wananchi watakuwa na
maradhi.
“Awamu ya Tano ilianza na
ujenzi wa vituo 44 vya afya na kufuatiwa na vituo 74 na sasa vituo takribani 120 vinaendelea kujengwa
maeneo mbalimbali ili kutimiza lengo la kuwa na Kituo cha Afya kwa kila Kata”,
alieleza Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji, alisema Serikali
imeweka utaratibu wa Kata ambazo zipo jirani kutumia kituo kimoja wakati lengo
kuu la kujenga kituo kimoja cha afya kwa kila Kata likiendelea kutekelezwa katika uongozi wa Serikali ya
Awamu ya Tano.
Aidha amebainisha kuwa
Sekta ya Afya inatazamwa kwa upana wake na ndio sababu Serikali inaboresha pia
miundombinu ya Maji ili wananchi waweze kupata maji safi na salama ili
kuimarisha Afya zao.
Mganga Mkuu wa Halmashauri
ya Mji wa Kasulu, Dkt. Mshana Dastan, amemweleza Dkt. Kijaji kwamba kukamilika
kwa majengo hayo mapya ya Kituo cha Afya Kiganamo, kutaimarisha utoaji wa huduma za
afya kwa kuwa, kinategemewa na idadi kubwa ya watu wanaotoka ndani na nje ya
Halmashauri ya Mji wa Kasulu.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Mji wa Kasulu, Bi. Fatina Laay, amesema kuwa wagonjwa katika
zahanati hiyo wamekuwa wakilala zaidi ya watatu kwenye kitanda kimoja na kwamba
kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo yaliyokamilika kwa zaidi ya asilimia 98
kutaondoa changamoto hiyo.
"Mbali na Serikali
kutupatia kiasi hicho cha shilingi milioni 500, mwisho mwa mwaka wa fedha
uliopita, Serikali imetupatia kiasi kingine cha shilingi milioni 400kwa ajili
ya ujenzi wa Kituo cha Afya Hedu Juu, kitakacho saidia kutoa huduma wa watu
walioko pembezoni" Alieleza Bi. Laay.
Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, yuko mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi kutembelea
na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayopatiwa fedha na Hazina pamoja na
kuzungumza na jumuiya ya wafanyabiashara.
No comments:
Post a Comment