WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema ukosefu wa uadilifu ni moja ya eneo ambalo
lilitia doa utendaji wa sekta binafsi hususan pale ambapo ilishirikiana
na Serikali.
Ameyasema
hayo leo (Jumanne, Agosti 28 ,2018) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 18
wa mwaka wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa niaba ya Rais
Dkt. John Magufuli.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar Es Salaam, Waziri Mkuu amesema uadilifu ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi na Serikali na TPSF.
“Katika kusisitiza suala la uadilifu, nitoe rai kwamba muwe na mfumo wa kujitathmini,kupeana alama chanya na kuhimizanakuenenda katika misingi bora ya uendeshaji wa shughuli zenu.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu ameitaka TPSF ijifunze kwa wenzao walioendelea kwa kutokuwa
na vitendo vya rushwa, kutoa adhabu kwa wanaoenda kinyume na misingi ya
uadilifu walijiwekea.
Amesema
kwa kufanya hivyo watakuwa wamejiongezea nguvu yao kama taasisi lakini
pia kupeleka ujumbe kwa wanachama wao kuwa wanathamini haki na kuchukia
rushwa.
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa shughuli za sekta binafsi zimeendelea kuongoza
katika kuchangia pato la Taifa na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.
Amesema
kwa mujibu wa takwimu sekta ya utalii inachangia asilimia tisa, huduma
asilimia 35, kilimo asilimia 26.6, madini asilimia 3.3 na sekta ya
viwanda inachangia takribani asilimia 10.
“Jukumu
letu sote ni kuchochea uzalishaji na kufanya wepesi kwa wajasiriamali
wetu watoke nje ya mipaka yetu na kwenda kuuza bidhaa zetu nchi jirani.
TPSF mtusaidie katika hili.”
Waziri
Mkuu amesema Serikali kwa upande wake itaendelea kuweka mazingira
wezeshi kwa kuboresha miundombinu, kutoa vivutio kwenye kodi, kanuni na
sheria ili kukuza sekta binafsi.
Hivyo,
Waziri Mkuu amesema sekta binafsi nchini nayo haina budi kutumia vema
fursa hiyo ya uwepo wa mazingira wezeshi na rafiki kwa kuwekeza kwenye
uchumi wa nchi.
Amesema
ni vema wakatambua kwamba wana jukumu kuliletea Taifa maendeleo, hivyo
wafanye kazi kwa ukaribu na ubia baina yao ili kuhakikisha nchi
inanufaika na fursa zilizopo.
Pia
amewasihi waendelee kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji wa bidhaa za
viwandani na wahakikishe kuwa wanajali maisha ya Watanzania ambao ndio
soko na wateja wa bidhaa zao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 28, 2018.
No comments:
Post a Comment