Na Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi nchini
limewahakikishia wananchi kuendelea kuwepo kwa hali ya usalama na Amani hapa
nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwepo kwa hali ya utulivu na usalama katika
chaguzi ndogo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu
wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro wakati akiwa
katika ziara katika Shule ya Polisi Moshi (CCP) ambapo aliweza kuzungumza na
Wakufunzi na Askari waliopo mafunzoni Chuoni hapo ikiwa na lengo la kukagua
mwenendo wa mafunzo yanayoendelea katika Vyuo vya Polisi nchini.
IGP Sirro amesema katika maeneo
yaliyofanya uchaguzi mdogo hali ilikuwa shwari licha ya kuwepo kwa matukio
madogo ambayo yanaendelea kushungulikiwa na upelelezi utakapokamilika majalada
yao yatapelekwa kwa Waendesha mashtaka kwa hatua zaidi.
“ Hali iliuwa shwari na ni
wazi kuwa wananchi sasa wameelewa umuhimu wa kutii sheria bila ya kushurutishwa na natoa rai waendelee kudumisha
hali hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za Wahalifu na uhalifu katika maeneo
yao” Alisema Sirro.
Katika hatua nyingine akiwa Shule ya Polisi Moshi zamani CCP
IGP Sirro alitoa pongezi zake kwa Walimu
na Uongozi kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuwapika Askari hususani katika
mafunzo yao ya awali ambapo ametaka kila Askari kutambua wajibu wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule
ya Polisi Moshi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Mungi
amesema Chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha
kuwa kila Askari anayetoka anakuwa na ukakamavu wa kutosha na nidhamu ya
kuwahudumia Wananchi licha ya kuwepo kwa Changamoto za madeni ya maji na umeme.
Alisema wanaendelea kuboresha
miundombinu ya Chuo hicho kwa kutumia miradi iliyopo ili kukiweka katika hali
ya usalama zaidi ikiwemo kujenga uzio imara kuzunguka maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment