HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 15, 2018

JNIA yajiimarisha katika usalama wa mizigo ya abiria

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inapenda kutoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu taarifa iliyosambazwa kupitia Mtandao wa Kijamii (Jamii forum) ya tarehe 13 Agosti 2018 yenye kichwa cha habari kinachosomeka “WARNING! Tahadhari ya WIZI kwa Wasafiri Uwanja wa JNIA”.  
 
Mwandishi wa taarifa hiyo anadai kupoteza komputa mpakato aina ya Mac Laptop katika moja ya mizigo yake wiki hii. 
 
Mamlaka inapenda kuufahamisha Umma kwamba taarifa iliyotolewa sio ya kweli na Watanzania wanatakiwa kuipuuza, kwa kuwa JNIA imejiimarisha katika usalama wa mizigo na abiria, hivyo Mamlaka inapenda kuufahamisha umma yafuatayo:-

     i.         Zoezi la Usimamiaji wa mizigo kwa abiria wanaosafiri (departure) na abiria wanaowasili (arrival) linafanyika kwa uangalizi na usimamizi mkubwa kutoka kwa Maafisa Usalama wa Kiwanja na wa kwenye ndege, ambayo abiria atasafiria au kuwasili nayo, pia maeneo yote ambayo mizigo ya abiria hupita yamefungwa kamera maalum za kiusalama (CCTV). 

   ii.         Hata hivyo, Mamlaka inapenda kuufanamisha umma kuwa Maafisa Usalama wanaokuwa kwenye mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo (scanner), hawawezi kuwasiliana na wafanyakazi wanaohusika na upandishaji wa mizigo kwenye ndege (loaders), kwa kuwa hawaruhusiwi kutumia simu za mkononi muda wote wa kazi na hufanya kazi chini ya usimamizi wa Msimamizi wa zamu wa eneo husika, ambalo pia limefungwa kamera kwa ajili ya usalama (CCTV) zinazorekodi kila tukio.

 iii.         Pia Mamlaka inapenda kuwafahamisha kwamba katika kipindi cha kati ya mwezi Julai na Agosti, 2018 kupitia kitengo chake cha Usalama kimepokea malalamiko mawili ya upotevu wa mizigo ya abiria,  ambapo tukio la kwanza ni la abiria mmoja kuweka komputa mpakato yake  (laptop) na Ipad kimakosa kwenye begi la abiria mwingine alipotoka kwenye ukaguzi na tayari ameshairudisha na mhusika kukabidhiwa mali yake; na tukio la pili ni la abiria aliyewasili kutoka nje ya nchi alidai amepotelewa na komputa mpakato, lakini baada ya ukaguzi wa kamera za usalama inaonesha eneo alilolalamikia hakutoa kifaa hicho na badala yake alitoa kadi ya Homa ya Manjano (Yellow Fever) pekee, hatahivyo uchunguzi unaendelea.

Hatahivyo, hakukuwa na tukio linalolalamikiwa la kuibiwa komputa mpakato (Mac laptop) wakati abiria huyo anayedai ametumia JNIA.

Mamlaka inatoa wito kwa watanzania wanaotumia kiwanja hiki na vingine vyote nchini vilivyopo chini ya serikali, kutoa taarifa kwa ndege husika wanaposafiri na vitu vya thamani na pia kuhakikisha utimilifu wa mizigo yao kabla hawajatoka katika eneo la Kiwanja cha ndege chochote, na abiria yeyote ambaye atagundua upotevu wa aina yeyote ya mali zake atoe taarifa kwa Maafisa Usalama katika eneo la Kiwanja kwa ajili ya msaada zaidi ikiwa ni pamoja na kuangalia picha zilizorekodiwa kwa muda wote na kamera maalumu ya kiusalama (CCTV).

Mamlaka inasimamia vyema Dira yake ya kuwa mtoaji Huduma za Viwanja vya Ndege kwa kiwango cha Kimataifa; na Dhima ya kutoa huduma bora na viwezeshi katika viwanja vya ndege kwa kuzingatia ufanisi katika matumizi ya rasilimali zilizopo. Mamlaka inasimamia viwanja vya ndege 58 vilivyopo chini ya serikali.
Imetolewa
Kitengo cha Uhusiano TAA

No comments:

Post a Comment

Pages