NA TIGANYA VINCENT, TABORA
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imetoa muda wa mwezi mmoja kwa Maofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya zote kuhakikisha wamekamilisha zoezi la kuwatambua na kuwapatia vitambulisho vya matibabu kwa wazee wote ambao wana umri wa miaka 60 kuendelea.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa
Tabora Aggrey Mwanri wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wazee Mkoani
humo na baada ya takwimu za waliopatiwa vitambulisho hadi sasa kuwa kidogo
wakati wazee wengi wakiwa bado hajapatiwa.
Alisema kati ya wazee 74,454 waliotambuliwa ni 26,000 ndio wameshapata vitambulisho hivyo
na kuongeza wengine bado hawajatambuliwa.
Mkuu huyo wa Mkoa alikasilishwa na Halmashauri
ya Manispaa ya Tabora kwa kutoa vitambulisho 100 kati ya Wazee 9,000
waliotambuliwa.
Mwanri alisema katika zoezi hilo la kuwatambua
na kuwapatia vitambalisho hakuna kumuacha mzee hata mmoja aliye na sifa kwa
mujibu wa Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003.
Alisema baada ya mwezi mmoja kupita Afisa Ustawi wa Jamii ambaye atakutwa katika Halmashauri
yake kuna wazee wenye sifa hawana vitambulisho ajue hana kazi.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tabora huyo aliwaagiza
Waganga Wakuu wa Wilaya (DMO) kuhakikisha kunakuwepo na dawa muhimu na madirisha
ya kuwahudumia wazee ili wasitumie muda mwingi kusubiri matibabu.
Alisema kitendo cha kuwachelewesha kinaweza
kuwasababisha matatizo kuwa makubwa na kuwepo na uwezekano wa kupoteza maisha.
Mwanri aliwashauri kutenga muda wa kuwahudumia
wazee katika maeneo yao na kuhakikisha wanafika Hospitali wanakuwa wa kwanza
kupata huduma.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika
Makungu alisema Serikali inawategemea sana wazee hao katika kutoa ushauri ili
watendaji wafanye maamuzi sahihi kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa
ujumla.
Alisema wazee ni kundi muhimu kwa watendaji wa
ngazi mbalimbali katika kuchotoa uzoefu kutoka kwao ili kuhakikisha Mkoa
unasonga mbele.
Awali Afisa Ustawi Mkoa wa Tabora Baraka
Makona alisema kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Wazee , Mabaraza ya Wazee
yatakiwa kuwa hadi ngazi za Mitaa na Vijiji.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Tabora
Shidumu Mathew aliishukuru Serikali kwa kuwajali na kuwaomba kusaidia kutatua
kero mbalimbali zinazowakabili kama vile kupata matibabu katika mazingira
rafiki.
Baraza la Wazee wa Mkoa wa Tabora linajumuisha
Mwenyekiti Shidumu Mathew, Makamu Mwenyekiti Maulidi Bakari, Katibu Humbi
Shija, Mweka Hazina Sadala Juma, Mjumbe Jumanne Rashid, Naomi Kaswaka na Mumbe Tatu
Ramadhan.
No comments:
Post a Comment