HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 14, 2018

USHIRIKIANO SEKTA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI KUIBUA MIRADI YA KIMKAKATI KUKUZA UCHUMI

Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said, akisalimiana na mwezeshaji wa mafunzo ya ubia kati ya Sekta za Umma na Sekta Binafsi Bw. Node Ned White kutoka Benki ya Dunia, katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga. 
Kamishna wa masuala ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. John Mboya akitoa maelezo mafupi kwa mgeni rasmi (hayupo pichani) kabla ya kumkaribisha kwa ajili ya ufunguzi  wa mafunzo ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa Watumishi wa Halmashauri mkoani Tanga.
Baadhi ya Washiriki wakifuatilia mafunzo ya ubia kati ya Sekta za Umma na Sekta Binafsi yaliyokuwa yakiendelea katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said, akifungua mafunzo ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafisi katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa Tanga ulio jumuisha watendaji mbalimbali kutoka Halmashauri 60 nchini.
Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said, (wa pili kulia), (wa kwanza kulia) ni Kamishna wa masuala ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. John Mboya, (wa kwanza kushoto) ni Afisa Sheria Mkuu wa PPP Bi. Flora Tenga (wa pili kushoto) ni Bw. Hemedi Mpili kutoka TAMISEMI wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ubia kati ya Sekta za Umma na Sekta Binafsi yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

Na Mwandishi Maalum, Tanga
Serikali imezitaka Wizara na Taasisi za Umma kuhakikisha zinawajibika kikamilifu kufuata hatua zote muhimu za utekelezaji wa miradi ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (Public Private Partinaship-PPP), kwa kuwa hatua hiyo itaiwezesha  Serikali kupata miradi ya maendeleo yenye sifa na ubora unaotakiwa nchini.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi  Zena Said alipokuwa  akifungua mafunzo ya siku tano ya ubia kati ya Sekta za Umma na Sekta Binafsi (PPP) kwa Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , Taasisi na Mashirika ya Umma nchini.
Alisema kuwa  utaratibu huo wa PPP ni njia bora ya kukabiliana na changamoto  mbalimbali ikiwemo ile ya kibajeti na kuiwezesha Serikali kuweza kufikia malengo yake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kutoa huduma bora na zenye  tija kwa wananchi wake.
Mhandisi  Zena aliongeza kuwa, iwapo Halmashauri nchini zitafuata utaratibu wa PPP kwa kubuni miradi yenye sifa stahiki  na kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango itasaidia kufikia malengo yake ya  kujitegemea.
“Kiukweli hili ni jambo la faraja na ni fursa kubwa kwa Halmashauri zetu kutumia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii hususani ujenzi wa hospitali za kisasa, miundombinu iliyobora”alisema Bi. Zena.
Mhandisi Zena alifafanua kuwa Tanzania tayari imenufaika na uwekezaji kwenye miradi ya PPP kwa kuhusisha jumla ya miradi 20 yenye thamani ya Dola za marekani  Milioni 863. 39.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na Mradi wa Uendeshaji wa Huduma ya Usafiri Jijini Dar es Salaam Awamu ya kwanza (UDART) ambao uko katika hatua ya utekelezaji.
Aliongeza kuwa, miradi mingine ambayo iko katika hatua za mwisho za uidhinishwaji wa upembuzi yakinifu ni pamoja na  Mradi wa Kuzalisha Madawa Muhimu na Vifaa Tiba, Mradi wa Ujenzi wa Vyuo Kumi (10) Vya Ufundi Stadi unaotekelezwa na VETA na Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa kutumia Gesi asilia- Somanga – Fungu unaoandaliwa na TANESCO.
 Aidha, aliongeza  kuwa kupitia mafunzo hayo  yatawasaidia wataalamu katika ngazi za Halmashauri  kuibua na kuandaa maandiko ya miradi ikiwemo  taarifa za upembuzi yakinifu.
“Kuandaa nyaraka za zabuni pamoja na mikataba ya PPP  na   kushiriki kikamilifu katika kufanya majadiliano na  mbia aliyeshinda zabuni kabla ya kuingia mikataba”. Aliongeza Mhandisi Zena.
Naye Kamishna wa PPP Dkt. John Mboya alisema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuzisaidia Halmashauri kuwajengea uwezo wa kujitafutia fursa za kiuchumi na kuachana na utegemezi wa bajeti kuu kwa ajili ya kushughuli za maendeleo.
Aidha aliziasa Halmashauri nchini kutumia fursa hiyo kutekeleza miradi ya kimaendeleo kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo  nchini ili  miradi hiyo iweze kuwa na tija katika kuchangia bajeti ya Serikali.
Mafunzo hayo yameshirikisha Halmashauri 60 nchini ambazo zinatekeleza miradi ya PPP ili kuwajengea uwezo wa kubuni na kuibua miradi ya ubia na kuwawezesha kuingia mikataba kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ambayo yanafanyika mkoani Tanga kwa muda wa siku tano.

No comments:

Post a Comment

Pages