HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 15, 2018

WAFANYABIASHARA KIGOMA WAIOMBA SERIKALI IONDOE GHARAMA ZA VIZA NA CHANJO MIPAKANI ILI KUKUZA BIASHARA

Na Benny Mwaipaja, WFM, Kigoma
Wafanyabiashara Mkoani Kigoma wameiomba Serikali kuondoa gharama za Cheti cha Matibabu na utaratibu wa Viza kwa nchi ambazo hazipo katika Jumuiya ya Afrika mashariki hasa kwa wafanyabiashara wadogo ili kuchochea biashara kati ya Mkoa huo na nchi jirani zikiwemo Burundi na Congo.
Hayo yamebainishwa Mkoani Kigoma wakati wa Mkutano kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, na Wafanyabiashara wa mkoa huo uliowakutanisha pia Madiwani wa Kigoma Ujiji na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe na viongozi wengine.
Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kigoma, Bw. Raymond Ndabhiyegetse, alisema kuwa Serikali imeweka gharama ya Viza ya Dola 50 na Dola 10 kwa ajili ya cheti cha chanjo kwa nchi ambazo si wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wadogo ambao ndio waliokuwa chachu ya biashara mkoani Kigoma.
Pause: Bw. Raymond Ndabhiyegetse-Katibu Jumuiya ya Wafanyabiashara-Kigoma
“Waliobaki katika biashara ni wafanyabiashara wakubwa ambao hununua bidhaa za jumla kutoka viwandani na kusababisha wafanyabiashara wadogo wa mkoa wa Kigoma kutonufaika na kusababisha mzunguko wa pesa na biashara kuwa mdogo ikilinganishwa na kipindi ambacho hakukuwa na masharti ya kulipia viza na chanjo”, alisema Bw. Ndabhiyegetse.
Aidha Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA),  Mkoani Kigoma, Bw. Prosper Guga, alisema kuwa matatizo mengine yanayodhoofisha biashara na kudidimiza uchumi wa Mkoa wa Kigoma unaopakana na Nchi ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  (DRC) ni  kutokuwepo kwa Benki za Kimataifa hususani nchini DRC jambo linalowafanya wafanyabiashara kutembea na fedha taslimu hivyo kuwa hatari kwa usalama wa fedha hizo kwa kuzingatia mazingira ya nchi wanzaofanyanazo biashara.
Pause Bw. Prosper Guga-Katibu Mtendaji-TCCIA-Kigoma
“Wizara ya Fedha na Mipango isaidie kuzishawishi Benki za Biashara kufungua matawi katika nchi za DRC, Burundi na nyingine ili kukuza zaidi biashara katika ukanda huu ambao una fursa kubwa za biashara” aliongeza Bw. Guga.
Kuhusu suala la Gharama za Viza na Cheti cha Matibabu, Bw. Guga aliitaka Serikali kuondoa utaratibu huo na badala yake cheti maalum cha ujirani mwema kitumike kama ilivyo mipaka mingine ya Goma- Rwanda na  Uvira-Bunjumbura.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ameishauri Serikali kuufanya mji wa Kigoma kuwa Bandari Kavu ili mizigo yote inayosafirishwa kwa treni kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kwa ajili ya kuivusha kwenda nchi jirani za Congo na Burundi, ianzie katika mji huo wa kibiashara ili kukuza ajira na uchumi wa mkoa huo
Pause: Mhe. Zitto Kabwe - Mbunge wa Kigoma Mjini
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa amefurahishwa na hoja za wafanyabiashara hao hivyo akaahidi kushirikiana na Wizara nyingine ikiweo ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na pia Wizara ya Mambo ya Ndani ili kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa haraka.
Pause: Dkt. Ashatu Kijaji-Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Congo mwaka 1991/92  walikubaliana kuwa  na soko na mahusiano mema kati ya Mkoa wa Kigoma na mikoa jirani ya Congo, lengo likiwa wafanyabiashara hao  kuuza bidhaa Kigoma na kununua bidhaa na mazao kwenda Congo hivyo kurahisisha wafanyabiashara wadogo kufanyabiashara na kuibua matajiri wakubwa katika kipindi cha mwaka 1990 hadi 2000.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji, amefanya Ziara ya Kikazi mkoani Kigoma ambapo ametembelea na kukagua miradi iliyopewa fedha na Serikali na pia kuzungumza na wafanyabiashara kuhusu uboreshaji wa mazingira ya biashara na ulipaji wa kodi.

No comments:

Post a Comment

Pages