Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisisitiza masuala ya
ubunifu na uadilifu kwa wafanyakazi wa TRA nchi nzima ili kuongeza mapato ya Serikali
kwa njia ya kodi bila kuwabughudhi walipa kodi na kukemea vitendo vya rushwa,
alipokutana na kuzungumza na wafanyakazi wa TRA, Jijini Tanga. Kulia kwake ni
Meneja wa TRA mkoani Tanga, Bw. Masawa Masawa.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (mbele), akizungumza
na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania TRA mkoani Tanga na kusisitiza umuhimu wa kudhibiti biashara ya
magendo katika mwambao wa Tanga ili kuongeza mapato ya Serikali.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (aliyeketi kulia), akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Tanga, baada ya kumalizika kwa mkutano wake na wafanyakazi hao, Jijini Tanga.
Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip Isdor Mpango ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA,
kuwachukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu wafanyakazi wake
wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo rushwa na kutumia
njia zisizokubalika wakati wa kukusanya kodi za Serikali.
Dkt. Mpango ametoa maelekezo
hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TRA Mkoa wa Tanga, ambapo ameagiza
wafanyakazi wawili wa mamlaka hiyo, Robinson Munisi na Abraham Maleko
waondolewe kwenye kazi wanazofanya sasa na kupangiwa kazi nyingine baada ya
kuwepo kwa tuhuma za ulevi wa kupindukia na kujihusisha na mtandao wa
wafanyabiashara unaotumika kuikosesha Serikali mapato yake
Amewataka watumishi wa mamlaka
hiyo kuwa waadilifu kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na lugha za kuudhi kwa
wateja wao ili kupunguza malalamiko kutoka kwa walipa kodi na kuonya kuwa
serikali haitomvumilia mtumishi yeyote atakayefanya kazi kinyume na maadili ili
kujenga nidhamu kwa watumishi hao na hatimaye kuongeza ufanisi katika
ukusanyaji mapato ya Serikali.
"Mwambieni Kamishna Mkuu
wa TRA (Bw. Charles Kichere) kwa watumishi hawa siwataki, wapelekeni maeneo
mengine mbali huko na muendelee kuwachunguza, na nataka kupata taarifa ya
watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo
kujihusisha na rushwa" alisisitiza Dkt. Mpango
Aidha, amemwagiza Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Charles
Kichere, kuhakikisha boti la doria katika Mwambao wa Bahari mkoani Tanga
linapatikana haraka ili kuzuia biashara ya magendo inayoyofanywa kwa kutumia
bandari bubu hivyo kuikosesha Serikali mapato yake.
"Ni lazima jambo hili
lifanyike haraka kwa sababu ya umuhimu wake kwasababu si tu kwamba Serikali
inapoteza mapato yake kutokana na vitendo hivyo vya kuvusha magendo kupitia
bandari bubu lakini pia ni hatari kwa usalama wa Taifa kwa sababu maadui
wanaweza kupitisha silaha" alionya Dkt. Mpango.
Akisoma taarifa fupi ya
utekelezaji wa majukumu ya Mamalaka hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Bw.
Masawa Masawa alisema makusanyo ya Mkoa huo yamekuwa yakiongezeka Mwaka hadi
Mwaka kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwaka 2013 hadi 2017 ambapo katika
Mwaka 2016/17 Mkoa ulikusanya Shilingi bilioni 107.39 kati ya Shilingi bilioni
131.06 ya malengo kwa Mwaka huo ambayo ni sawa asilimia 82 ya makusanyo.
Kuhusu maadili ya wafanyakazi
wa Mamlaka hiyo mkoani Tanga, Bw. Masawa amesema kuwa pamoja na kuwapa elimu
kuhusu maadili mema kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU,
wamekuwa wakiwachukulia hatua kali watumishi wao wanaobainika kujihusisha na
vitendo vinavyochafua taswira ya mamlaka hiyo.
Akihitimisha mkutano huo, Dkt.
Mpango, alimwagiza Meneja huyo kupandisha kiwango cha ukusanyaji mapato kwa
asilimia 100 na kutoa onyo kwa Mameneja
wote wa TRA nchini watakaoshindwa kufikia lengo hilo wajitathmini kama wanatosha
kwenye nafasi zao.
No comments:
Post a Comment