*Asema ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 katika kila mkoa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema hadi
kufikia Juni, 2018 jumla ya viwanda 1,596 vimejengwa ambapo ni sawa na
asilimia 61.4 ya lengo la kujenga viwanda 2,600 hadi Desemba 31, 2018
ikiwa ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 katika kila mkoa.
Ameyasema
hayo leo (Alhamisi, Septemba 27, 2018) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa
34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais
Dkt. John Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya
Mrisho Kikwete, jijini Dodoma.
Waziri
Mkuu amesema kuwa viwanda hivyo vimejengwa kupitia agizo la Waziri wa
Nchi OR- TAMISEMI kwamba kila Mkoa ujenge viwanda 100.
Amesema
tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuelekea uchumi wa
viwanda, inaonesha kwamba mpaka sasa jumla ya hekta 367,077 zimetengwa
katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya viwanda vikubwa,
viwanda vya kati na viwanda vidogo.
“Nitoe
wito kwenu kwamba mwendelee kupiga hatua nyingine mbele zaidi katika
hili, tujue katika hekta hizo zilizotajwa ni kiasi gani kimerasimishwa
kwa viwanda vipi, bidhaa zipi zinazalishwa, hali ya miundombinu ikoje na
kuna mikakati gani ya kuiendeleza. Pia tufahamu ni ajira ngapi
zilizozalishwa kutokana na uanzishwaji wa viwanda hivyo.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewaagiza viongozi na wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwawezesha wananchi
kushiriki katika kubuni na kusimamia miradi ya maendeleo na kuibua fursa
za uwekezaji.
Pia
kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo na vikubwa ili Tanzania iweze
kufikia lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Tumieni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kuwawezesha
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia vikundi vyao ili wawekeze
katika viwanda vidogo vidogo vyenye kuleta tija na kuongeza pato la
kaya ili kuutokomeza umaskini.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali katika Dira ya
Maendeleo ya 2025 ni kuhakikisha Halmashauri zinakuwa na uwezo wa
kujitegemea kimapato kwa zaidi ya asilimia 80 ifikapo 2025.
Amesema
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili
kuhakikisha lengo hilo linatimia. Serikali imeanzisha utaratibu wa
kugharamia miradi ya kimkakati yenye lengo la kuziongezea halmashauri
mapato ya uhakika na kupunguza utegemezi wa ruzuku.
“Hadi
sasa, sh. bilioni 131.5 zimeidhinishwa kutekeleza miradi ipatayo 22
katika halmashauri 17 zilizokidhi vigezo kwenye mikoa 10. Hivi
ninavyozungumza, tayari kiasi cha sh. bilioni 16.4 zimekwishapelekwa
kwenye halmashauri hizo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi
iliyokusudiwa.”
Waziri
Mkuu amesema kuwa uchambuzi wa miradi mingine zaidi unaendelea na
halmashauri zitakazokidhi vigezo zitapata fedha kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi hiyo.
Amesisitiza
kwamba fedha hizo zikatumike kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa na si
vinginevyo. Amesema kwa sasa, hatutakuwa na utaratibu wa kutoa fedha
bila kufahamu kwa kina fedha hizo zinakwenda kufanya nini na zitaleta
mabadiliko gani.
“Nimesikia
kwamba katika baadhi ya halmashauri fedha zilizokwishatolewa bado
hazijaanza kutumika kikamilifu watu wanaendelea kujadili namna ya
kuzitumia, niwakumbushe tu kwamba Mheshimiwa Rais hakutoa fedha hizo ili
zikakae benki. Wakurugenzi wa Halmashauri mlisaini makubaliano ya
matumizi ya fedha hizo, hivyo, zingatieni hilo.”
Waziri
Mkuu amewataka Madiwani wasimamie matumizi ya fedha hizo ili
halmashauri zipate miradi yenye ubora unaotakiwa, inayolingana na kiasi
cha fedha kilichotolewa pamoja na inayokamilika kwa wakati.
Kauli mbiu ya Mkutano huo wa 34 inasema “Umuhimu
wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Kutoa Huduma na Ushiriki wa
Wananchi Kupitia Fursa na Vikwazo Kuelekea Uchumi wa Viwanda”.
Amesema
kauli mbiu hiyo, inatilia mkazo maneno ya awali ya Rais Dkt. Magufuli,
kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zipo karibu zaidi na wananchi na
zinapaswa kutoa huduma na kuwashirikisha wananchi katika kujiletea
maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma
ALHAMISI, SEPTEMBA 27, 2018.
No comments:
Post a Comment