*Asema lengo ni kuziwezesha halmashauri kujiendesha zenyewe
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amesema kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano
kwa sasa ni kuboresha maeneo ya utawala kwa lengo la kutekeleza miradi
ya maendeleo na kuongeza uwezo wa halmashauri kujiendesha zenyewe.
Ameyasema
hayo leo (Alhamisi, Septemba 27, 2018) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa
34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais
Dkt. John Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya
Mrisho Kikwete, jijini Dodoma.
Ametoa
kauli hiyo baada ya kuwepo kwa maombi mengi ya kuanzisha maeneo mapya
ya utawala nchini. “Kama mnakumbuka nimekuwa nikieleza mara kadhaa
kwamba tunazishukuru Serikali za Awamu zilizotangulia kwa kuainisha
maeneo ya utawala.”
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanapaswa wajitathmini sambamba
na kuainisha mikakati mizuri ili kuhakikisha lengo la kusogeza huduma
kwa wananchi linatimia.
Waziri
Mkuu amesema katika kipindi cha mwaka 2014/15 jumla ya halmashauri 66
na mkoa mmoja wa Songwe vilianzishwa pamoja na vijiji 1,949, mitaa 1,379
na vitongoji 8,777. Hadi sasa, maeneo hayo hayajaweza kuwa na
miundombinu, vifaa na watumishi wa kutosha ili kuwezesha wananchi kupata
huduma iliyokusudiwa.
“Mathalani,
mkoa wa Songwe halmashauri zake zote, hata halmashauri ya wilaya ya
Mbozi ambapo ndiyo makao makuu ya mkoa bado haujafikia vigezo vya kuwa
Manispaa. Baadhi ya halmashauri zinaendelea na ujenzi wa ofisi wakati
nyingine kama Mafia, Rufiji, Handeni na Ludewa zipo kwenye magofu na
huwezi kuamini kama ni Ofisi za Halmashauri.”
“Taarifa
nilizonazo hadi sasa ni kwamba tayari sh. bilioni 120.7 zimepokelewa
kwenye halmashauri mbalimbali kati ya sh. bilioni 238.8 zinazohitajika
kukamilisha ujenzi wa majengo ya halmashauri sawa na asilimia 50.54 ya
fedha zote.
Amesema
kiasi kilichobaki kitaendelea kutolewa kupitia bajeti ya Serikali na
mapato ya ndani ya halmashauri, ambapo baadhi yake zitapewa fedha za
kukamilisha ujenzi baada ya uhakiki kwa sababu zimekuwa zikipokea fedha
kwa muda mrefu.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa halmashauri hizo wahakikishe
wanajenga Ofisi za Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji badala ya
kuendelea kuanzisha Serikali hizo huku zikiwa hazina hata ofisi.
Kuhusu
uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za
Mitaa, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na zoezi la kuajiri
watumishi hususan wa kada za afya na elimu, ambapo kati
ya mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 Serikali imeajiri watumishi wa kada
ya elimu 13,472 na afya 8,238 kwa lengo la kuziba mapengo yaliyopo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma
ALHAMISI, SEPTEMBA 17, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu mitambo ya umeme
kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tekinolojia na Masoko wa REA,
Elineema Mkumbo (wapili kushoto) wakati alipotembelea banda la maonyesho
la REA kabla ya kufungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za
Mitaa Kwenye ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma, Septemba 27,
2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya
Tawala za Mitaa (ALAT) kwenye ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini
Dodoma Septemba 27, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa
(ALAT) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua
Mkutano huo kwenye ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma,
Septemba 27, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Picha ya pamoja.
PMO 9097 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na baadhi ya viongozi
walioshiriki katika Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa
(ALAT) Kwenye ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma Septemba 27,
2018. Kulia ni Mwenyekiti wa ALAT, Gulaam Hafeez 'Mukadam', wapili
kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge na wanne kulia
ni Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment