HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 20, 2018

Viwanja vya ndege nchini vyapongezwa kwa utoaji bora wa huduma

Na Mwandishi Wetu
 
IKIWA zimepita siku kadhaa tangu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma za wizi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mtanzania aishie nje ya nchi amejitokeza na kuipongeza TAA kwa ubora wa huduma ambazo inatoa kwa watumiaji wa uwanja huo.

Mtanzania huyo aliyefahamika kwa jina la Bw. Barnabas Kijika ameipongeza TAA kwa taarifa nzuri ambayo imeitoa kwa Umma kuhusiana na suala la kupotelewa mizigo kwakuwa hata yeye alishawahi kupotelewa mizigo JNIA lakini alipofuatilia alipata yote ikiwa haijaibiwa.

“Mimi nasikia moyo wa kuishukuru TAA na wafanyakazi wote kwa sababu hata mimi hili suala hilo limewahi kunitokea kipindi nimekuja Tanzania nikitokea nchi za Uarabuni ambapo mizigo miwili ikawa imepotea.

Lakini nikatoa maelezo kwa wahusika na baada ya siku moja nikapigiwa simu kupitia namba niliyoacha kwa ajili ya kupewa taarifa kwamba mizigo yangu imepatikana na nilipoikagua nikakuta mizigo yangu ipo salama yote hakuna kilichopotea,” amesema Bw. Kijika.

Pia Bw. Kijika amesema siku za nyuma alishughudia baada ya siku moja upatikanaji wa mizigo ya watalii wawili waliokuwa wakisafiri kupitia JNIA baada ya taarifa ya kupotea kwa mizigo hiyo kuwafikia wafanyakazi wa JNIA.

Katika sehemu ya barua pepe ambayo Bw. Kijika alituma kupitia anwani ya info@airports.go.tz na sauti aliyojirekodi na kuirusha kwa njia ya Whatsapp amebainisha kwamba, kwa muda mrefu amekuwa akitumia viwanja mbalimbali vya ndege vya Tanzania na changamoto ambazo anaziona ni za kawaida.

 “Kwa zaidi ya miaka 15 nimekuwa nikitumia airports za Tanzania sijawahi kujuta isipokuwa changamoto za kawaida hata Ulaya zipo,” amebainisha Bw. Kijika.

Hivi karibuni abiria mmoja Mtanzania mwenye asili ya Kiarabu alilalamikia kuibiwa pochi lenye fedha na vitambulisho mbalimbali wakati akisafiri kupitia JNIA kwenda nchi za Falme za Kiarabu, ambapo hata hivyo Kaka yake, Bw. Wael Hassan alipooneshwa picha zilizopigwa na kamera za usalama (CCTV), walikiri hakuna uwizi wowote na ndugu yao hakuibiwa na aliomba radhi kwa niaba ya ndugu yao huyo.

No comments:

Post a Comment

Pages