HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 20, 2018

WAZIRI MKUU AAGIZA WATAFITI WA ZAO LA UFUTA WAPELEKWE MAKUTUPORA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba apeleke wataalamu kwenye kituo cha utafiti kilichopo Makutupora, Dodoma ili wazalishe mbegu bora za ufuta kwa ajili ya mikoa ya kanda ya kati.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Alhamisi, Septemba 20, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mauno, wilayani Kondoa ambako alienda kukagua ujenzi wa kituo cha afya. Waziri Mkuu leo ameanza ziara ya kikazi ya siku saba katika mkoa wa Dodoma.

Alikuwa akijibu ombi la mbunge wa viti maalum, Bi. Mariam Ditopile ambaye alisema mkoa wa Dodoma ni wa pili kwa uzalishaji wa ufuta hapa nchini lakini aina ya ufuta inayozalishwa ni ya daraja la chini kwa sababu hawana mbegu za ufuta mweupe.

“Ili mradi mikoa ya kanda ya kati inazalisha ufuta, ninamuagiza Waziri wa Kilimo ahamishe watumishi kutoka kokote ili wakae Makutupora na kuwasaidia wakulima wawe na mbegu bora zenye kutoa mafuta mengi,” alisema.

Amesema kila mwaka Serikali inatumia zaidi ya dola za Marekani milioni 267 kuagiza mafuta ya kula kutoa nje ya nchi na kwamba hivi sasa imeamua kufufua mazao ya mbegu za mafuta ili mafuta ya kula yazalishwe kwa wingi hapa nchini.

 “Sasa hivi tumeanza kufufua mazao ya mbegu za mafuta ni nilianza mkoa wa Kigoma kwa kuhimiza kilimo cha michikichi. Sasa hivi niko Dodoma nahimiza ufuta na alizeti na nitaenda Singida kwa ajili ya zao hilo la alizeti,” amesema.

Kuhusu bei ya zao hilo, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Binilith Mahenge awasiliane na wakuu wa mikoa ya Lindi na Mtwara ili kubaini mbinu walizotumia kuhimiza zao hilo lakini pia amemtaka asimamie kwa karibu na ahakikishe kuwa katika msimu ujao, uuzaji wa zao hilo unafanyika kwa njia ya minada ili wakulima waweze kupata bei nzuri.

“Acheni kuuza ufuta nyumbani. Tabia ya mnunuzi kumfuata mkulima nyumbani ni wizi mtupu. Uzeni ufuta kwa minada, uzeni ufuta kwa minada. Kama mnataka hela, uzeni ufuta kwa minada,” amesisitizia wananchi hao.

“Ni kazi ya maafisa kilimo na maafisa ushirika wa wilaya kusimamia zao hili ka karibu. Wabainishe maghala ya kuhifadhia mazao huko huko wilayani ili wakulima wakishavuna, mnarekodi mavuno yao, mnapanga tarehe ya mnada mapema ili wananchi wawepo na wanunuzi wawepo pia,” amesema.

Amewataka wananchi hao walime kwa wingi zao la alizeti kwa sababu lina bei nzuri na halina gharama kubwa za maandalizi. “Nimeambiwa kulima ekari moja hapa Mauno ni sh. 30,000; kila ekari inatumia kilo tano na kila kilo moja ya mbegu ni sh. 500/- ukiweka na palizi kama sh. 30,000/- gharama zote ni sh.62,500/-,” amesema.

“Ukivuna ekari moja unapata magunia 20, na kila gunia linatoa dumu moja la lita 20. Kwa magunia yote utapata madumu 20, na kila dumu linauzwa sh. 60,000/- kwa hiyo una uwezo wa kupata sh. milioni 1.2 kwa ekari moja. Ukitoa gharama zako, bado unabakia na sh. 1,137,500/-. Sasa ukilima ekari mbili au tatu hali itakuwaje?” alihoji Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Kondoa ambako atazungumza na wananchi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, SEPTEMBA 20, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages