Na Veronica Simba–Mara
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema
Serikali kupitia Wizara anayoisimamia, imejipanga kuhakikisha wawekezaji wote
katika sekta ya madini wanatumia umeme katika shughuli zao ili wazalishe kwa
tija itakayowawezesha kulipa kodi stahiki kwa Taifa na hivyo kukuza uchumi wa
nchi.
Alitoa kauli hiyo, Septemba 18, 2018 mkoani Mara,
wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa Adam Malima ofisini kwake, kabla ya kuanza
ziara ya kazi katika Mkoa huo, kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
umeme.
“Tunataka migodi izalishe kwa tija ili kusudi ilipe
kodi, ushuru na tozo zote stahiki kwa Serikali hivyo kukuza uchumi wa nchi
yetu.”
Kauli hiyo ya Waziri Kalemani, aliitoa kufuatia ombi
la Mkuu wa Mkoa kuhusu kuupatia nishati ya umeme Mgodi wa Dhahabu wa Nyamongo
uliopo mkoani humo; ambapo Waziri Kalemani alimhakikishia kuwa Wizara yake
inakamilisha taratibu za kuunganisha umeme katika Mgodi huo ndani ya muda
mfupi, baada ya mwekezaji huyo kukamilisha malipo.
Alisema kuwa, tayari alishamwagiza Meneja wa TANESCO
wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Emmanuel Kachewa kuhakikisha Mgodi huo unaunganishiwa
umeme kabla ya mwezi huu kuisha.
Waziri Kalemani alisema kuwa kwa muda mrefu, wengi wa
wawekezaji katika sekta ya madini wamekuwa wakitumia mafuta katika kuendesha
mitambo hiyo hivyo kulalamika kwamba wanatumia gharama kubwa inayowasababishia
hasara katika uzalishaji hivyo kushindwa kulipa kodi stahiki za Serikali kadri
ipasavyo.
Alifafanua kuwa, ni kwa sababu hiyo, Serikali
imedhamiria na ilikwishaanza kutekeleza mpango wa kuhakikisha wawekezaji wote
wa sekta husika, wakiwemo wakubwa, wa – kati na hata wadogo wanatumia umeme ili
kuondoa visingizio vya kuendesha shughuli zao kwa hasara na hivyo kutokulipa
kodi ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani ametoa wito kwa
taasisi zote zinazodaiwa na TANESCO, kuendelea kulipa madeni yao ili
kuliwezesha shirika hilo la umma kuwahudumia watanzania kwa viwango na ubora.
“TANESCO isipolipwa madeni inayozidai taasisi na hata
wateja binafsi, inapata shida kuwahudumia wateja wake ambao ni Watanzania.
Kwahiyo, tunahamasisha wote ambao bado hawajalipa Ankara za umeme kuendelea
kulipa ili kuipunguzia Serikali mzigo,” alisisitiza.
Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani alitembelea maeneo
mbalimbali ambapo aliwasha umeme katika vijiji vya Nyakatende, Musoma Vijijini
na Bubombi kilichopo Wilaya ya Rorya pamoja na kuzungumza na wananchi.
Aidha, alitembelea kijiji cha Nyamohonda kilichopo
wilayani Tarime, mpakani mwa Tanzania na Kenya na kuwaahidi wananchi kuwa
watapata huduma ya umeme hivi karibuni kwani tayari kazi hiyo imekwishaanza
kutekelezwa.
Awali, akiwasilisha kwa Waziri taarifa ya utekelezaji
wa miradi ya umeme katika eneo lake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mara, Mhandisi
Emmanuel Kachewa alisema kuwa jumla ya vijiji 273 vitapatiwa umeme kupitia
Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Sehemu ya Kwanza (REA III – Phase 1),
ambao umekwishaanza kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2019.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha
Bubombi, Wilaya ya Rorya mkoani Mara, muda mfupi kabla ya kuwasha rasmi umeme
katika eneo hilo. Hafla hiyo ilifanyika Septemba 18, 2018.
Meneja
wa TANESCO Mkoa wa Mara, Mhandisi Emmanuel Kachewa akiwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani humo, kwa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipowasili katika
Mkoa huo kwa ajili ya ziara ya kazi Septemba 18, 2018.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasha umeme katika nyumba ya mmoja wa
wakazi wa Kijiji cha Nyakatende, Musoma Vijijini, ikiwa ni ishara ya uwashaji
rasmi wa nishati hiyo katika eneo hilo. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi
mkoani humo, Septemba 18, 2018 kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
No comments:
Post a Comment