WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kujenga mradi
wa kuzalisha umeme kwenye maporomoko ya mto Rufiji, Stiegler’s Gorge utasaidia
sana kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini.
Akizungumza
baada ya kutembelea eneo utakapojengwa mradi huo, leo (Alhamisi, Oktoba 4,
2018), Waziri Mkuu amesema umeme utakaotokana na maji, utazalishwa kwa gharama
nafuu na utakuwa wa uhakika zaidi.
Amesema
kwa vile umeme utakaozalishwa katika mradi wa Stiegler’s Gorge utakuwa wa bei nafuu
na hivyo kuwa rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini, utatumika kama nishati
mbadala kwa kuni na mkaa ambao umechangia sana kwenye uharibifu wa
mazingira hasa ukataji miti.
Waziri
Mkuu Majaliwa amewaomba viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wawaelimishe
Watanzania kuwa mradi wa Stiegler’s Gorge una faida kubwa kwa Taifa kiuchumi na
hauna athari za mazingira na badala yake utayaboresha.
Amewahakikishia
Watanzania kuwa mradi huo utajengwa na utakamilika katika muda
uliokusudiwa ambao ni miezi 36 kuanzia siku mkandarasi atakapokabidhiwa kazi
hiyo.
Akizungumzia
usalama katika eneo la mradi, Waziri Mkuu amesema viongozi wa mikoa ya Morogoro
na Pwani wahakikishe kwamba wanaweka ulinzi wa kutosha kuanzia sasa na
wakati ujenzi utakapoanza ili kuzuia hujuma na vitendo
vya wizi na udokozi vinavyoweza kuvuruga kasi ya ujenzi wa mradi.
Amesema
vifaa vitakavyoletwa na mkadarasi lazima vilindwe na wajenzi watakaoshiriki
katika ujenzi wa mradi wahakikishiwe usalama wao na mali zao.
Amewataka
wananchi pia washiriki katika ulinzi kwa kutoa taarifa kwa vyombo
vya dola kuhusu watu wenye mienendo inayoweza kuzorotesha ujenzi wa mradi huo
kwani jukumu la ulinzi si la polisi peke yao.
Kuhusu ajira
kwa vijana wanaotoka katika maeneo yanayozunguka mradi, Waziri Mkuu amesema
utaratibu utawekwa ili vijana wenye sifa wapewe nafasi ya kushiriki kwenye
usaili na ikibidi watafanyiwa mchujo kwenye maeneo yatakayofikiwa
na wengi.
Aliwaasa
wote watakaobahatika kupata ajira ya kushiriki katika ujenzi wa mradi huo wawe
waadilifu na wachapakazi ili kulinda heshima ya vijana wa Kitanzania na kuwashawishi
wajenzi wa mradi kuajiri vijana wengine zaidi.
Kuhusu Wizara
ambazo zinaguswa na maandalizi ya ujenzi wa miundombinu inayohitajika
katika ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge, Waziri Mkuu ameagiza wizara hizo
zishirikiane ili kuhakikisha kwamba kila Wizara inatimiza majukumu
iliyopangiwa kwa wakati.
Wizara
ambazo tayari zimeanza kuweka miundombinu wezeshi kwa mradi huo ni pamoja na
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inayosimamia ujenzi wa barabara na
tawi la reli itakayounganisha eneo la mradi na stesheni ya Fuga
katika reli ya TAZARA kazi ambayo imeanza na Waziri Mkuu wenyewe aliikagua.
Wizara
ya maji nayo tayari imetimiza jukumu lake la kupeka maji katika eneo la mradi
wakati wizara ya nishati imepeleka umeme. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi pamoja na Wizara ya Kilimo nazo zipo kwenye eneo la mradi kutimiza
majukumu yote yanayozigusa.
Awali, Waziri wa Nishati,
Dkt. Medard Kalemani aliishukuru Serikali kwa kukubali kutoa fedha ambazo zimesaidia
sana katika ujenzi wa miundombinu ya maandalizi ya ujenzi wa mradi.
IMETOLEWA NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI,
OKTOBA 04, 2018.
No comments:
Post a Comment